Alhamisi, Julai 17, 2014

TRAFIKI 27 WATIMULIWA KAZI TANZANIA

Jeshi la Polisi nchini Kikosi cha Usalama Barabarani limewafukuza kazi askari 27 baada ya kubainika kujihusisha na vitendo vya rushwa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza nidhamu, uwajibikaji na maadili ya kazi kwa askari polisi wa barabarani nchini.
Askari hao wamefukuzwa kazi kuanzia Januari mwaka huu ambapo uamuzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa usimamizi wa nidhamu na mapambano dhidi ya rushwa baada ya baadhi ya askari wa jeshi hilo kudaiwa kujihusisha zaidi na vitendo hivyo.
Ni katika mkutano na waandishi wa habari ndipo Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mohamed Mpinga anasema usimamizi huo dhidi ya vitendo vya rushwa umesaidia ongezeko la ukamataji wa makosa na mabadiliko ya nidhamu za madereva kwenye matumizi ya barabara.
Akatoa tathmini ya ajali za barabarani na kubainisha Mikoa iliyoongoza kwa ajali nyingi kuanzia Januari mwaka huu ni Dar Es Salaam yenye ajali 5,052 Morogoro ajali 514 huku Kilimanjaro ikiwa na ajali 332.
Hata hivyo hali ya ukamataji wa makosa kwa madereva wasiopenda kutii sheria bila shuruti yameongezeka kulinganisha na mwaka jana ambapo Januari hadi Juni mwaka huu yamebainika makosa 515,677 huku Januari hadi Juni mwaka jana yakiwa 301,404 ikiwa ni ongezeko la makosa 214,273 sawa na asilimia 71.

0 comments:

Chapisha Maoni