Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
Jumatatu Julai 14, 2014 amekutana na kundi la wasanii kutoka Marekani
lililowasili nchini usiku wa Alhamisi, Julai 10, 2014, kwa ajili ya
kuendesha mafunzo kwa wasanii wa Tanzania kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BOT) mjini Dar es Salaam.
Wasanii hao
ni pamoja na Terrence J. (Jenkins), mwendeshaji wa kipindi cha muziki
kwenye televisheni ya E! Entertainment, mwigizaji wa filamu na mtunzi wa
vitabu na Revi Shelton, Mtendaji wa Shughuli za Muziki katika Kampuni
ya Outlet Media Group.
Wengine ni
Chaka Zulu, Mtendaji wa Shughuli za Muziki kutoka Kampuni ya Disturbing
The Peace Records na Davis Banner, mwigizaji, mwanamuziki, mtunzi na
msimamizi wa shughuli za muziki ambaye amepata kushinda tuzo maarufu ya
Grammy.
Kiasi cha
wasanii 250 walishiriki semina hiyo inayoitwa Mafunzo ya Uendelezaji
Usanii. Hiyo ilikuwa ni kutimiza ahadi aliyotoa Rais Kikwete kwa wasanii
wa Tanzania kuwa atachangia kuinua kiwango cha ujuzi na weledi wao kwa
kuwaandalia mafunzo yatayoendeshwa na magwiji wa sanaa kutoka Marekani
sasa imetimia.
Akizindua
Kampeni ya Uzalendo kwa Vijana inayoendeshwa na Muungano wa Wasanii
Tanzania kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma mwezi uliopita, Juni 14,
2014, Rais Kikwete aliahidi kuchangia kuinua kiwango cha usanii na
weledi wa wasanii wa Tanzania kwa kusaidia kuandaa mafunzo
yatakayoendeshwa na wasanii maarufu kutoka Marekani.
Mbali na
kuendesha shughuli za mafunzo ya wasanii ambazo wamekuwa wakizifanya kwa
makundi madogo madogo tokea walipowasili nchini, pia wanamuziki hao wa
Marekani na kundi la wapiga picha watatembelea sehemu mbali mbali
nchini, hasa kwenye vivutio vya watalii, ambako watapiga picha na
kuandaa vipindi vya kuitangaza Tanzania katika vyombo vya habari vya
Marekani.




0 comments:
Chapisha Maoni