Rais mpya wa Malawi, Peter Mutharika, aliyeapishwa kuingia rasmi
madarakani hapo jana amesema nchi sasa itatafuta marafiki wapya katika
kuisadia nchi hiyo. Amesema nchi hiyo ambayo imekuwa siku zote
ikizitegemea nchi za Magharibi kwa ufadhili itabadili mwelekeo na
kuzijongelea China na Urusi. Mutharika aliitoa kauli hiyo katika sherehe
za kuapishwa kwake zilizosusiwa na rais aliyeondoka madarakani, Joyce
Banda, baada ya kushindwa katika uchaguzi huo uliozusha utata. Mutharika
aliyeingia madarakani katika nchi hiyo ambayo ni miongoni mwa nchi
masikini kabisa duniani ambako asilimia 40 ya bajeti yake inatokana na
msaada wa wafadhili amesema nchi wafadhili zinakaribishwa kubakia
Malawi. Hata hivyo rais huyo amebaini kwamba sera za kigeni za taifa
hilo zitazingatia maslahi ya nchi hiyo huku akiweka wazi kwamba uhusiano
uliokuwepo awali utaendelea. Uingereza na Marekani zimetoa ahadi ya
kushirikiana na serikali hiyo mpya ya Mutharika. Aidha rais huyo wa
Malawi amezungumzia kusikitishwa kwake na hatua ya rais aliyeondoka
madakani, Joyce Banda, ya kukataa kufika kumkabidhi madaraka ingawa kwa
upande mwingine msemaji wa Bibi Banda amesema kiongozi huyo hakualikwa
rasmi katika sherehe hizo na juu ya hilo aliondolewa msafara rasmi
unaoandamana na rais punde baada ya Mutharika kutangazwa mshindi wa
uchaguzi wa rais siku ya Jumamosi.
0 comments:
Chapisha Maoni