Jumapili, Juni 01, 2014

FANYA HAYA KUMPATA MCHUMBA MWENYE MAPENZI YA KWELI

KWANZA- Ni ya mwanamke/mwanaume mwenyewe kujifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi anayemhitaji katika maisha yake. Ifahamike kuwa kila mwanaume ana wake na kila mwanamke anaye wake wa maisha pia. Hivyo asiyekufaa wewe anawafaa wengine, kinachotakiwa ni wewe kujitambua kwanza ili umtambue umtakaye.
Wanawake/wanaume wengi hawafahamu wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila kujua wanataka kununua nini? Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa mapenzi, wakachezewe na kuumizwa moyo bure.
PILI- Ni kuketi chini na kuorodhesha vigezo stahili vya mwanaume/mwanamke unayemtaka. Baada ya hapo orodhesha tena kasoro za mwanaume/mwanamke unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi kuzivumilia kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu hajakamilika, ana upungufu wake.
TATU- Anza kumsaka kwa kutumia milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni kuruhusu macho yawaone wanaume/wanawake na kuwatathmini kwa maumbile yao ya nje na kisha kupata majibu kutoka moyoni juu ya kuvutia kwao ambako hutambulika kwa moyo kurithika na mwili kusisimka.
NNE - Kuanzisha safari ya kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo. Hapa suala la ukaribu baina ya mwanaume na mwanamke linahitajika. Msingi unaotajwa hapa ni kujenga mazoea ya kawaida yasiyokuwa na masuala ya kimapenzi na ngono. Kutambuana, dini, viwango vya elimu, kabila na makundi ya marafiki ni mambo ya kuzingatia.
Katika uchunguzi huu mwanamke/mwanaume anayetafuta mpenzi hana budi kupitia na kumlinganisha huyo aliyempata na vigezo alivyojiwekea. Zoezi hili liendane na kuweka alama ya pata kila anapobaini kuwa mwanaume/mwanamke anayemchunguza amepata moja ya vigezo vyake. Lakini pia aweke alama ya kosa kwa kila kasoro anayoivumilia na ile asiyoivumilia.
TANO - Ajipe muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza huyo mwanaume, kisha aketi chini na aanze kujumlisha alama za vigezo alivyovijiwekea na jinsi mwanaume huyo alivyopata au kukosa.
Ikibainika mwanaume aliyechaguliwa amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo vilivyowekwa, basi ujue kuwa anafaa. Kuhusu alama chache alizikosa anaweza kusaidia kuzikamilisha polepole wakati wa maisha ya ndoa.
Lakini angalizo kubwa kabisa ni kwamba mwanaume/mwanamke akionekana kuanguka katika kasoro zisizoweza kuvumilia kwa zaidi ya alama tatu. Yaani kwa mfano ni mlevi, mwizi, muongo, mbishi na katika hizo kashindwa 3, huyu hafai, ni vema akawekwa kando kwani huwezi kubeba kero 3 kwa pamoja katika maisha.
SITA - Kusajili mapenzi yenye malengo yanayotekelezeka. Lazima baada ya kuchunguzana kwa kina wapenzi watengeneze muongozo wa mapenzi yao. Wasiwe kama wanyama, lazima mipango ya wapi wametoka walipo na wanapokwenda.
Hata hivyo watalaam wanasema lazima wapenzi wapime umakini wao kwa vitendo. Kama wamekubaliana kuoana, suala la mume kwenda kujitambulisha kwa wakwe na hatua ya kuiendea ndoa ionekane. Usiri usiwepo tena. Kila mmoja amuone mwenzake kama sehemu ya maisha yake na mara zote wasaidiane kwa ukaribu.

0 comments:

Chapisha Maoni