Alhamisi, Februari 06, 2014

WANANCHI WAFUNGA BARABARA MOROGORO, POLISI WAWASHA MOTO

MABOMU ya machozi yametumika kuwatawanya wakulima wa eneo la Melela, Mvomero mkoani Morogoro waliokuwa wamefunga barabara ya Iringa - Morogoro wakimtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera aende kusuluhisha mgogoro uliopo baina yao na wafugaji.
Wakulima hao wanadai kuwa wenzao watano jana wamevamiwa na wafugaji wa kabila la Wamasai na kuwajeruhi vibaya kwa vitu vyenye ncha kali sehemu za siri na kupelekea kulazwa katika Hospitali ya Mkoa Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka alifika eneo hilo ambapo wananchi hao walikuwa wamechoma matairi na kusababisha msongamano mkubwa wa magari yaendayo Iringa na yale yaelekeayo Moro lakini wakulima hao walikataa kumsikiliza wakimtaka mkuu wa mkoa.
Baada ya vurugu kuwa kubwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile aliwaaamuru vijana wake wawatawanye wakulima hao ambao waligoma na kuanza kuwapiga kwa mawe kitendo kilichopelekea polisi kupiga mabomu ya machozi na kufanikiwa kuwatawanya.
Wananchi takribani 20 wamekamatwa na polisi katika vurugu hizo.
Kwa sasa hali kidogo imetulia na magari yameanza kupita eneo hilo.

0 comments:

Chapisha Maoni