Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na mashirika mawili ya WIN na Gallup
mwishoni mwa mwaka uliomalizika juzi wa 2013 umeonesha kuwa, watu wengi duniani
wanaitambua Marekani kuwa ndio tishio kubwa zaidi la amani duniani.
Kituo cha habari cha Newsmax kimenukuu matokeo ya uchunguzi wa maoni wa
Gallup na Win na kutangaza kuwa kwa mujibu wa matokeo hayo asilimia 24 ya watu
walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wameitaja Marekani kuwa ndio tishio
kubwa zaidi la amani ya kimataifa.Ripoti ya Newsmax imesema kuwa, hata asilimia 13 ya Wamarekani wanaamini kuwa nchi yao ni hatari kwa amani ya kimataifa. Uchunguzi huo wa maoni ni matokeo ya uchunguzi wa fikra za watu katika nchi 63 duniani ambao ulifanyika katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Novemba mwaka uliomalizika wa 2013.
Vilevile matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika la Pew yameonesha kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa katika kipindi cha miaka 40, asilimia 70 ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa, nafasi ya nchi yao imeporomoka ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita na kwamba Marekani haina heshima na hadhi kama iliyokuwa nayo miaka ya huko nyuma. Vilevile asilimia 56 ya Wamarekani walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wamesema nchi yao inapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu masuala yake yenyewe.




0 comments:
Chapisha Maoni