Hatimaye baada ya kusubiriwa kwa muda, hatua ya kwanza ya
makubaliano ya nyuklia ya Geneva kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na
kundi la 5+1 imeanza kutekelezwa leo.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh_2hZkAN8TXHaJZDMg9vAioFSqlJkVt6J55nmGBe6mGXcYY663d7ZIvEhcNyrJJ98zHSCqBCt3_jMhFAbAvYFCcDtsdTmvpkvmzu1Q5FjU85ix17ZlHaFSBxCrdVrQqPsVJv0XgEds4sSO/s1600/1c04410219d2ef6596cde89b19c86614_XL.jpg)
Wasimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki pia
waliwasili nchini Iran Ijumaa iliyopita kwa ajili ya kusimamia
utekelezaji wa hatua kwa hatua wa makubaliano hayo. Kwa msingi huo
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa hiari yake itahifadhi nusu ya urani
iliyorutubishwa kwa asilimia 20 kwa ajili ya kuzalisha nishati ya
tanurinyuklia ya utafiti ya Tehran na nusu inayobakia itabadilishwa na
kuwa urani iliyorutubishwa kwa asilimia 5. Iran pia itatangaza kuwa
katika kipindi cha miezi sita ijayo ya awamu ya kwanza ya utekelezaji wa
makubaliano ya Geneva haitarutubisha unanium kwa zaidi ya asilimia 5.
Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran Ali Akbar Salehi amesema
kuwa hatua muhimu zaidi ya kwanza inayochukuliwa na Iran ni kusimamisha
kwa hiari urutubishaji wa madini ya urani kwa asilimia 20 ambao unaanza
leo katika vituo vya Natanz na Fordow. Salehi amesema urutubishaji wa
madini ya urani kwa asilimia 20 haukuwa kabisa katika ajenda za nyuklia
za Iran lakini wataalamu wa nyuklia hapa nchini walichukua uamuzi wa
kurutubisha urani kwa kiwango hicho baada ya kumalizika nishati ya kituo
cha utafiti cha Tehran na wakati Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya
Atomiki (IAEA) ulipokataa kutekeleza majukumu yake ya kudhamini nishati
hiyo.
Sambamba na hatua hizo zinazochukuliwa na Iran, Umoja wa
Ulaya pia hii leo umeanza kupunguza na kuondoa vikwazo vyake dhidi ya
Iran. Kwa mujibu wa hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mkataba wa Geneva
vikwazo vyote vya petrokemikali dhidi ya Iran vitaondolewa. Vilevile
nchi hizo zitaiondolea Iran vikwazo vya dhahabu, madini mengine yenye
thamani na usafirishaji.
Kwa utaratibu huo mwenendo wa kutatua hitilafu juu ya faili
la nyuklia la Iran ambalo lilianzishwa bila ya sababu yoyote umeanza
leo kwa kuanza kutekelezwa awamu ya kwanza ya makubaliano ya Geneva.
Hatua hii kwa hakika itathibitisha nia njema ya pande mbili ya
kutekeleza ahadi zao.
0 comments:
Chapisha Maoni