Alhamisi, Januari 23, 2014

RIPOTI KAMILI JUU YA KIFO CHA MBUNGE WA CHALINZE, BWANAMDOGO

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepata pigo lingine kwa kuondokewa na Mbunge wa Chalinze (CCM), Said Bwanamdogo, ambaye amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Bwanamdogo alifariki dunia jana katika wodi ya Taasisi
ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) alikokuwa akitibiwa.
Msemaji wa Moi, Jumaa Almasi alisema Bwanamdogo alifariki saa moja asubuhi jana na mwili wake umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuongoza Watanzania kesho katika mazishi ya mbunge huyo kijijini kwake Miono, Kata ya Miono wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alisema kwa sasa msiba huo upo Makondeko jijini Dar es Salaam na taratibu zinafanyika kuhamishia mwili wa marehemu kijijini kwake kwa shughuli nyingine za maziko.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu jijini Dar es Salaam, baba mdogo wa marehemu, Omar Nguya alisema kuwa mwili wa mbunge huyo utazikwa kesho kijijini hapo.
Nguya alisema kuwa kabla ya mwili wa mbunge huyo kusafirishwa, kutakuwa na shughuli ya kuaga kitaifa itakayofanyika kesho kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Anne Makinda ameeleza kusikitishwa na kifo cha Bwanamdogo.
Taarifa ya Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa ilisema kuwa mipango ya mazishi inaendelea kufanywa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya marehemu.
Hali ya mbunge huyo ilianza kubadilika tangu mwaka juzi, ambapo alisafirishwa kwa matibabu zaidi nchini India.
Bwanamdogo alitibiwa huko kwa zaidi ya miezi tisa, kabla ya kurejeshwa nchini baada ya familia yake kuomba aendelee na matibabu akiwa hapa nchini. Marehemu ameacha mjane na watoto sita.
Bwanamdogo ni mbunge wa pili kufariki tangu kuanza kwa mwaka huu akimfuatia Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa, aliyefariki dunia Januari Mosi, katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini ambako alikuwa amelazwa.

0 comments:

Chapisha Maoni