KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi amesema
hataki kuzisikia wala kuzungumzia habari za Simba na Etoile du Sahel kwa
kuwa hana mpango wa kurejea alikotoka.
Okwi ametoa tamko hilo ikiwa ni siku chache mara baada ya kupewa
‘kifungo’ cha muda, huku uongozi wa Yanga ukisisitiza kuwa utamtumia
mchezaji huyo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya
Komorozine ya Comoro inayotarajiwa kuchezwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Okwi
ambaye ni raia wa Uganda, alisema yeye ni mchezaji wa Yanga na mapenzi
yake yapo klabuni hapo, ndiyo maana hataki kuzungumzia suala la mgogoro
wa usajili wake, kwa kuwa hana mpango wa kurudi alipotoka.
“Najua baada ya muda TFF itaniruhusu kucheza, sitaki kurudi
nilipotoka kwa kulizungumzia suala la Etoile (du Sahel), pia sitaki
kuizungumzia Simba kwa kuwa siyo klabu yangu.
“Naipenda Yanga na mapenzi yangu yote yapo hapa, ndiyo maana leo hii
nipo klabuni nikiwa mchezaji wao. Nilikuwa tayari kuanza kuichezea Yanga
katika ligi hii (mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara) na Ligi ya Mabingwa
Afrika,” alisema Okwi.
Akizungumzia juu ya sakata la kuzuiwa kwa Okwi, Katibu Mkuu wa Yanga,
Beno Njovu ameliambia gazeti hili kuwa, watamtumia Okwi katika mechi
dhidi ya Komorozine kwa kuwa wamepata ruhusa ya kumtumia kutoka
Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).
“Caf wametupa ruhusa ya kumtumia, sisi tunawaamini wao, kwani
inavyoonekana TFF ndiyo hawamtaki (Okwi) kwenye ligi yao, sisi tunajua
Caf ni wakubwa kuliko TFF, hivyo tutamtumia siku hiyo.
“TFF hawakutupa muda wa kujitetea walipomsimamisha Okwi, tulianza
kuona taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, baadaye ndiyo wakatupa
barua, kwa hiyo Okwi tutaanza kumtumia rasmi kwenye mechi dhidi ya
Komorozine,” alisisitiza Beno.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema anaamini
tayari Fifa watakuwa wameshateua jaji wa kusikiliza kesi ya mchezaji
huyo.
“Hatuna shida ya kuwaandikia barua ya kuwauliza Fifa kile
kinachoendelea, tarehe ya awali iliyowekwa ni Januari 27, mwaka huu
waliyotakiwa kuwa wametulipa fedha za usajili lakini hawajafanya hivyo,”
alisema Kamwaga.
0 comments:
Chapisha Maoni