Jumanne, Januari 07, 2014

BAADA YA DAWASCO KUWAKATIA SANA WATU MAJI, NAYO YAKATIWA UMEME NA TANESCO KUTOKANA NANI KUBWA

Kibao cha operesheni kata maji kimeligeukia Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) baada ya kukatiwa umeme na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ikidaiwa Sh7 bilioni.
  Mmoja wa wafanyakazi katika mtambo wa Ruvu Chini, Mlandizi ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji, alisema kuwa umeme ulikatwa juzi katika mtambo huo kuanzia saa tatu asubuhi na ulirejeshwa saa mbili usiku.
Alisema limekuwa jambo la kawaida umeme kukatwa katika mtambo huo na kurudishwa baada ya mazungumzo baina ya watendaji wa juu wa Tanesco na Dawasco na mara ya mwisho ilikuwa miezi miwili iliyopita.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alikiri Dawasco kudaiwa kiasi cha Sh6.3 bilioni na kwamba Tanesco ilikata umeme kwa takriban saa saba juzi.
“Lakini waliurudisha jioni baada ya kuzungumza nao na wakatuelewa,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema ameiagiza Dawasco kuandaa programu ya namna ya kulipa deni hilo na kulimaliza.
“Tumezungumza nao (Tanesco) na mazungumzo bado yanaendelea ila nilichowaagiza Dawasco ni kwamba waweke programu ya namna ya kulilipa deni hilo. Hayo ndiyo maagizo yangu,” alisema Profesa Maghembe.
Hali hiyo inaaminika kuwa ndiyo imekuwa ikisababisha kukosekana mara kwa mara kwa maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumzia athari za kukatiwa umeme, mfanyakazi huyo wa Dawasco Ruvu Chini alisema: “Kuna wakati mwingine shirika hutangaza upungufu wa maji kwa madai kuwa kuna marekebisho yanafanyika na kuna wakati huwa haitangazwi kabisa lakini ukweli ni kwamba umeme hukatwa mara kwa mara na Tanesco.
“Watu wanaweza wakahisi labda maji hayatoki kutokana na mgawo usioeleweka wa Dawasco au wakati mwingine kudhani kuwa pengine ni kutokana na matatizo ya miundombinu, lakini ukweli ni kuwa kuna tatizo baina ya Tanesco na Dawasco.”
Tanesco watoa msimamo
Kaimu Meneja wa Tanesco, Adrian Severin alisema walifikia hatua hiyo kutokana na kuidai Dawasco Sh7 bilioni na kwamba kwa takriban mwaka mzima uliopita, shirika hilo halikulipa gharama zozote za huduma.

0 comments:

Chapisha Maoni