Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa amewataka waendesha
bodaboda na watu wengine wasimwite Rais kwa sababu wanamtengenezea chuki
na uhusiano mbaya na watu.
“Mbona mnataka kuniletea uchuro! Mnanitengenezea
ugomvi na watu jamani…,” alisema wakati akizindua Shirikisho la Bodaboda
Tanzania jana kwenye Viwanja vya Leaders, Dar es Salaam.
Lowassa amekuwa akitajwa kuwania urais katika
uchaguzi ujao wa Rais na wabunge utakofanyika 2015. Hatua hiyo imekuja
baada ya Lowassa kuwaeleza kuwa atafanya harambee ya kuchangisha fedha
ili kila aliyeingia kwenye shirikisho la waendesha bodaboda aweze kupata
pikipiki yake.
Baada ya kauli hiyo waendesha bodaboda hao
walipaza sauti zao wakiimba rais,rais …..wa mwaka 2015 huku wakidai
amepita hana mshindani. Aliwataka kuacha kumwita rais kwa sababu
wanamtengenezea ugomvi na watu.
Alisema asilimia 50 ya madereva wanaoendesha
bodaboda hizo siyo pikipiki zao hivyo kutokana na hilo atafanya harambee
ili kila mmoja kumiliki pikipiki yake ili waweze kujiajiri wenyewe.
“Tumeona kuna tofauti kubwa kati ya matajiri na
maskini hivyo nimeona kwenye shirikisho hili asilimia 50 siyo za kwenu.
Nimekusudia kuanzisha harambee ya madereva ambao hawana pikipiki ili
nao wawe nazo waweze kujiajiri,” alisema Lowasa.
Lowasa aliitaka Kamati ya Shirikisho la Bodaboda
kukutana naye Januari 15 mwaka 2014 ili kupanga harambee hiyo ifanyike
lini na wapi.
Alisema matajiri nchini wapo wengi nitawafuata na
kuwachangisha harambee wakiwemo Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald
Mengi na mfanyabiashara maarufu Said Salum Bakhresa.




0 comments:
Chapisha Maoni