Jumatano, Desemba 11, 2013

HOTUBA YA OBAMA AFRIKA KUSINI YAITIKISA DUNIA

Licha ya kuwa ni siku ya huzuni kwa dunia nzima, hotuba ya Rais wa Marekani, Barack Obama imewagusa maelfu ya watu waliokuwa kwenye Uwanja wa FNB katika ibada ya kitaifa kumwaga Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Obama aliyetumia dakika 20 katika hotuba yake iliyokuwa ikikatizwa na kelele za kumshangilia, aliwataka vijana wa Afrika na dunia nzima kuiga maisha aliyoishi Mandela kama yeye alivyojifunza mambo mengi kutoka kwa mzalendo huyo.
“Miaka 30 iliyopita nikiwa mwanafunzi, nilisoma Kitabu cha Mandela na tangu siku hiyo nilijifunza, nikajenga roho ya uthabiti. Iliamsha uwajibikaji kwa ajili yangu na kwa ajili ya watu wangu... hakika Mandela amenifanya niwe hivi nilivyo leo. Michelle na mimi tumenufaika sana na Mandela,” alisema Obama na kuongeza:
“Mandela alinifanya niwe mtu ninayesimama mbele yenu leo, alichangia kunifanya kuwa kiongozi bora. Nitaendelea kuiga mfano wake,”
Katika sherehe hizo, Obama alipokewa kwa shangwe na kushangiliwa kila alipopita na kila alipozungumza tofauti na ilivyokuwa kwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma ambaye alikuwa akizomewa.

Obama alimtaja Mandela kama kiongozi anayefaa kuigwa kwani pamoja na kukaa gerezani kwa miaka 27 akipigania uhuru, hakutaka kung’ang’ania madaraka na badala yake alistaafu kwa hiari yake, tofauti na viongozi wengi wa Afrika.

0 comments:

Chapisha Maoni