Shirikisho la Soka la Uturuki limewatia hatiani wachezaji wawili
wa kimataifa kutoka Ivory Coast Didier Drogba na Emmanuel Eboue
wanaosakata kabumbu kwenye klabu ya Galatasaray ya nchini Ururuki kwa
kosa la kuonyesha heshima na kumuenzi hayati Nelson Mandela, baada ya
kumalizika mechi ya ligi ya nchi hiyo.
Magazeti ya Milliyet na Hurriyet yanayochapishwa Uturuki yameandika
kuwa, Drogba anakabiliwa na kosa hilo baada ya kumalizika mechi kati ya
klabu yake ilipopambana na SB Elazigspor siku ya Ijumaa. Drogba alivua
jezi na kubakisha fulana ya ndani iliyosomeka maandishi "Thank You
Madiba". Taarifa zinasema kuwa, Eboue naye anakabiliwa na kosa kama hilo
ambapo yeye fulana yake ya ndani iliandikwa 'Rest in Peace Nelson
Mandela'.
Nelson Mandela alikuwa kiongozi aliyepambana na utawala wa ubaguzi wa
rangi nchini Afrika Kusini, na alifariki dunia Alhamisi iliyopita
akiwa na umri wa miaka 95. Shirikisho la Soka la Uturuki limetangaza
kuwa, wachezaji hao wawili watakabiliwa na adhabu ya utovu wa nidhamu
kwa kuvunja sheria ya shirikisho hilo inayokataza wachezaji kuvaa fulana
zinazotoa jumbe na nara za kisiasa.



0 comments:
Chapisha Maoni