Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, haina
hudima za maji kwa wiki moja sasa, jambo linalowalazimisha ndugu wa
wagonjwa kuingia wodini wakiwa na vidumu vya maji.
Tatizo hilo limekuja baada ya Mamlaka ya Majisafi
na Majitaka jijini Dar es Salaam (Dawasco ), kusitisha huduma hizo ili
kuruhusu uunganishaji wa mtambo mpya wa maji katika hospitali hiyo.
Mwandishi wa habari hii, jana alishuhudia ndugu wa wagonjwa waliolazwa
katika hospitali hiyo kubwa nchini, wakiwa na madumu ya maji
wakiwapelekea wagonjwa wao.
Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa walisema maji
yalikatwa Novemba 7 mwaka huu na kwamba hatua hiyo imesababisha
mazingira kuwa machafu na hasa vyooni, jambo linalohatarisha maisha yao.
Mmoja wa wagonjwa hao, Subira Ahmed, alisema tatizo hilo ni kubwa na kwamba linawalazimisha ndugu kubebewa maji kutoka nyumbani.
Alisema hata hivyo maji wanayoletewa na ndugu hayatoshelezi mahitaji.
“Sijaoga na leo (jana) nina siku ya tatu na hii
inatokana na ukweli kwamba maji tunayotumia tunanunua maana sisi ni
wageni kutoka Tabora”alisema Subira
Mgonjwa Lemeck Isaya, alisema vyoo wanavyotumia
viko katika hali mbaya kutokana na kukosa maji. Aliishauri Serikali
kuangalia uwezekano wa kuchimba visima virefu katika hospitali hiyo ili
kumaliza kero ya maji.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, alisema walitangaziwa kuwa Dawasco itakata huduma za maji.
Alisema hata hivyo maji kidogo yanapatikana kutoka katika kisima kilichopo katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Dawasco, Jackson Midala alisema
maji yalikatwa Novemba 9 mwaka huu kwa sababu walikuwa wanatengeneza
mtambo mpya wa maji.



0 comments:
Chapisha Maoni