Ijumaa, Oktoba 04, 2013

ZAMBIA YARIDHIA KATAZO LA VIROBA MBEYA

Serikali ya Zambia imeunga mkono tangazo la kupiga marufuku  uuzwaji  wa pombe kali zilizofungwa kwenye vikaratasi vya nailoni maarufu kama viroba.
Hivi karibu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro , kwa niaba ya Kamati ya Ulinzi na Usalama, alipiga marufuku uuzwaji wa pombe kutoka Zambia na Malawi  akisema zinaharibu nguvu kazi na kusababisha kero nyingi kwa vijana.
Pombe hizo za viroba zilizopigwa marufuku ni pamoja na; Double Punch, Power No 1, Boss, Royal Punch na   Charger.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais wa Jimbo la Muchinga nchini Zambia,  Charles Sipanje akiwa jijini Mbeya juzi,  alisema pombe hizo, zilishapigwa marufuku kutengenezwa nchini mwao.
Sipanje alisema, viroba hivyo maarufu kwa jina la ‘Tujilinjili’ nchini Zambia, vinauzwa Tanzania baada ya watengenezaji wake kupata soko la nje.
“Sisi tunaruhusu pombe za aina hiyo ziwe kwenye chupa kubwa na siyo karatasi. Hivyo ni halali kwa viongozi wa Mbeya kupiga marufuku,’’ alisema.
Pombe kali zilizofungwa kwenye karatasi hizo zinadaiwa kuuzwa kwa  kati ya Sh100 na Sh 700, jambo linalosababisha watu wengi, wakiwamo watoto na madereva kunywa bila kuzingtia taratibu na sheria za nchi.
Tayari vifo kadhaa vinavyodaiwa kusababishwa na pombe za aina hiyo  vimeripotiwa, kikiwamo cha hivi karibuni ambapo mtu mmoja alifariki baada ya kunywa pombe nyingi kwenye mkesha wa Mbio za Mwenge, wilayani Rungwe.

0 comments:

Chapisha Maoni