Alhamisi, Oktoba 31, 2013

VIJANA MILIONI 2.6 WANAISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI NCHINI TANZANIA

Vijana milioni 2.6 wenye umri wa miaka kati 15 na 24 nchini, wanaishi na virusi vya Ukimwi. Takwimu hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,  Sayansi na Utamaduni (Unesco), Abdoul Coulibaly,  wakati wa uzinduzi wa ripoti  ya elimu ya jinsia na  afya ya uzazi kwa vijana katika nchi 21 za Mashariki  na Kusini  mwa Afrika.
Karibu vijana 50 katika nchi hizo huambukizwa virusi vya Ukimwi kila saa moja, huku idadi ya wasichana wakiongoza kwa maambukizi hayo.
Coulibaly amesema idadi hiyo ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vijana kwa Tanzania, inachangiwa  na kutokuwapo kwa elimu ya kutosha ya jinsia  pamoja na VVU na Ukimwi, afya ya uzazi na ukuaji wa binadamu.


Amesema asilimia kubwa ya vijana hawana uelewa wa  masuala ya afya ya uzazi na jinsia, jambo ambalo husababisha kujiingiza  kwenye mapenzi katika umri mdogo na kusababisha kuongezeka kwa mimba za utotoni.

Pia ameiomba serikali kuweka mikakati madhubuti ya kutoa elimu ya afya na jinsia kwa vijana kwa ajili ya kusaidia kupunguza idadi ya maambukizi kwao pamoja na mimba za utotoni zinazosababishwa na ukosefu wa elimu hiyo.

Kaimu Mkurugenzi, kitengo cha masuala mtambuka kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Laetitia Sayi, amesema changamoto ya maambukizi ya VVU kwa vijana ni kubwa na kwamba serikali kwa upande wake inafanya jitihada mbalimbali za kutatua tatizo hilo.

0 comments:

Chapisha Maoni