Inawezekana kuwa kesi dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta katika
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ikaanza mwaka ujao badala ya mwezi
ujao wa Novemba kama ilivyokuwa imepengwa awali.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa waendesha mashtaka wa ICC wamesema hawapingi pendekezo la kuakhirisha kesi hiyo.
Viongozi wa Umoja wa Afrika wamekuwa wakishinikiza kesi hiyo
isikilizwe nchini Kenya na wengine wakitaka iakhirishwe kwa muda wa
mwaka mmoja. Aidha baadhi ya viongozi wa Afrika wametoa wito kwa rais wa
Kenya asifike mbele ya ICC kwa msingi kuwa mahakama hiyo inawalenga tu
Waafrika na kupuuza mamlaka ya kujitawala Kenya.
Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto wanakabiliwa na tuhuma za
kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ambapo watu
1,200 walipoteza maisha.
Kesi dhidi ya Kenyatta imepata pigo mara kadhaa baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka kujiondoa.



0 comments:
Chapisha Maoni