Ndugu Wananchi;
Wakati nikiwa safarini, tarehe 21 Septemba,
2013 kulitokea shambulilizi la kigaidi katika Jengo la Biashara la
Westgate, huko Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza maisha na zaidi
ya 200 walijeruhiwa. Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa
Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo
pamoja nao katika wakati huu wa majonzi.
Nafahamu kuwa baada ya tukio hilo watu wengi
hapa nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama wetu. Ni hofu ya msingi
kwani tarehe 8 Agosti, 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na
magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia walipoteza maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la
mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na
usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali. Tunaendelea
kujiimarisha bila kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama
wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi zetu
hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.
Baada ya tukio la Kenya, vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na
kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea
nchini. Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri
yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na
wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye
shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa
n.k. waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao. Pia waangalie
uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). Najua
watu wanaweza kulalamikia usumbufu au gharama, lakini gharama na hasara ya
kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.
Ndugu Wananchi;
Nawaomba muendelee
kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje msiache kuwa makini na kuchukua
tahadhari. Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama wanapoona mtu au
watu au kitu cha kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama wake, wa kila mtu,
jamii na taifa. Maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama
wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za
kuchukua. Sisi Serikalini tumejipanga kuchukua hatua zaidi kuimarisha
ulinzi na usalama wa nchi yetu na watu wake.



0 comments:
Chapisha Maoni