Abiria hamsini na moja waliokuwa wakisafiri na basi la Taqwa kutoka
Bujumbura na kuelekea jijini Dar-es-Salaam wametekwa katika kijiji cha
Milade wilayani Mkalama na kuporwa mali , simu na fedha zaidi ya
shilingi milioni mia mbili hamsini.
Akieleza kamanda wa polisi mkoani Singida bwana
Godfrey Kamwela amesema watekaji hao waliwaamrisha abiria kushuka chini
ya basi baada ya kuvunja vyoo na kuanza kuwasachi na kufanikiwa kupora
simu, fedha za kitanzania shilingi milioni tano ,dola za kimaerekani
dola laki moja elfu sitini na faranga zenye thamani ya elfu ishirini
kufuatia tukio hilo kamanda Kamwela amewaomba wananchi na makampuni ya
simu kushirikiana na jeshi la polisi ili kuweza kuwa kamata watu ambao
wamefanya tukio hilo.
Kwa upande wake dereva la basi hilo bwana Ahamed
Seif amesema gafla aliona majani barabarani na alipoangalia vizuri
aliona kuna mawe makubwa mawili yakiwa barabarani na kushindwa
kuyakwepa ,baada ya kugonga mawe hayo magurudumu yote mawili ya mbele
yalipasuka na gari ikaserereka umbali wa mita mia moja.
Kwa upande wao abiria na majeruhi wamesema waliona
gari likipoteza mwelekeo na baadaye walisikia sauti za watu zikiwaambia
washuke na watoe fedha na simu zao,lakini abiria wengine wametupia
lawama kwa wafanyakazi wa basi hilo kuchukuwa abiria wa njiani wakati
basi likiwa limejaa na abiria hao inasadikiwa ndio waliokuwa
wakiwasiliana mara kwa mara na watekaji.
Naye mganga wa wodi ya majeruhi ya hospitali ya
mkoa wa Singida Dkt Banuba Deogratias amesema walipokea majeruhi kumi
na tisa walikuwa na mipasuko na majeraa ya kupigwa na fimbo, wameweza
kuwatibu na kuruhusiwa isipo kuwa wengi wao hawana fedha kwa sababu ni
raia kutoka nchi za Burundi na Kongo walikuwa wakisubiri kukabidhiwa
kwa idara ya ustawi wa jamii ili wasaidiwe nauli za kurudi makwao.



0 comments:
Chapisha Maoni