Jumatatu, Septemba 16, 2013

BIBI NA BWANA WAUAWA MBEYA SABABU YA WIVU WA KIMAPENZI


Watu wawili wamefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa  kupigwa  mawe na marungu sehemu mbalimbali za miili yao huko Ituha, wilaya ya Mbeya Mjini mkoani na jijini Mbeya jana majira ya saa saba usiku.
Habari toka kwa maafisa wa polisi zinaeleza kuwa waliouawa ni mwanamke aliyetambulika kwa jina moja la Sophia anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35-40, Msafwa, mkulima na mkazi wa Ituha pamoja na mwanaume ambaye hajatambulika aneyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40-45.
Taarifa zinaeleza kuwa wawili hao wamefariki dunia wakati wakiwa njiani kupelekwa hospitalini baada ya kushambuliwa kwa kupigwa mawe na marungu sehemu mbali mbali za miili yao na mtu/watu wasiojulikana ambao waliwavamia wakiwa njiani  kurejea nyumbani usiku huo.
Aidha chanzo cha mauaji hayo kimetajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi na mpaka sasa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Zebedayo John, 32, Msafwa, mkulima na mkazi wa Ituha  tayari anashikiliwa na jeshi la polisi baada ya kutiliwa shaka kuhusika na tukio hilo lakini upelelezi bado unaendelea.
Pamoja na hayo kamanda wa polisi  mkoa wa Mbeya, kamishna msaidizi wa jeshi la polisi Diwani Athumani anatoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria badala yake watumie njia za mazungumzo kumaliza migogoro yao. Vile vile ametoa rai kwa yeyote aliye na taarifa juu ya waliko wahusika wa tukio hilo wazitoe ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.

0 comments:

Chapisha Maoni