Alhamisi, Agosti 08, 2013

NGASA AISHANGAA SIMBA

Winga wa Yanga, Mrisho Ngasa amesema uamuzi wa Simba kumjumuisha kwenye orodha ya wachezaji wake msimu ujao, siyo tu umemsikitisha, bali pia kumshangaza.



Mwanzoni mwa wiki hii, Simba ilipeleka majina ya wachezaji 28 watakaocheza timu hiyo msimu ujao likiwemo pia jina la Ngasa, ambaye klabu ya Yanga ilimsajili haraka baada ya kumalizika msimu uliopita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ngasa alisema ameshangazwa na uamuzi huo kwa vile yeye siyo tena
mchezaji wa Simba tangu baada ya kumalizika msimu uliopita.
Ngasa alijiunga na Simba kwa mkopo akitoka Azam FC, ambapo alicheza msimu mmoja kabla ya Yanga kumrejesha tena kuvaa jezi za rangi ya njano na kijani.
Ngasa alisema anashangazwa na hatua ya Simba kupeleka jina lake Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku wakifahamu kuwa yeye siyo mchezaji wao tangu msimu uliopita.
“Kuna vitu sipendi kuvizungumza sana, lakini kwa Simba kunifanya mimi mchezaji wao wakati siyo, inashangaza sana,” alisema Ngasa bila kutaka kuongelea suala hilo kwa kirefu.
“Sina tatizo na timu hizi mbili, lakini nashangazwa na Simba. Sina deni nao, sasa sielewi kwa nini wanafanya hivyo,” aliongeza Ngasa.
Viongozi wa timu zote mbili hivi karibuni walikaririwa kila upande ukidai mchezaji huyo ni mali yake.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajiwa kukutana Agosti14 kupitia majina yote ya wachezaji. Kama itabainika mchezaji amejisajili mara mbili, anaweza kufungiwa kucheza soka.

0 comments:

Chapisha Maoni