Serikali ya Japan imesema ina mpango kabambe wa kukuza uchumi wa
Tanzania, ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa duniani za Honda na
Panasonic kujenga viwanda vitakavyokuwa matawi yake hapa nchini.
Uamuzi na msimamo wa Japan umetangazwa jana jijini
Dar es Salaam na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa nchi hiyo,
Toshimistu Motegi alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya
Kikwete, Ikulu.
Taarifa ya Ikulu iliyosambazwa na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, ilimnukuu Motegi akisema: “Kwa kuanzia kampuni
mbili za Honda na Panasonic zimekubali kujenga viwanda nchini, kimoja
kwa ajili ya kutengeneza pikipiki za Honda na kingine kwa ajili ya
kutengeneza vifaa vya umeme.”
Akaweka msisitizo: “Huu ni mwanzo tu Mheshimiwa
Rais (Kikwete) kwa sababu kama nilivyosema kuwa tunataka Tanzania kuwa
nchi ya mfano ya uwekezaji wa Japan katika eneo hili la dunia, na namna
hiyo kwa pamoja tutakuwa tumeshirikiana katika kuongeza ajira kwa
wananchi wa Tanzania.”
Waziri huyo pia alisema kuwa baadhi ya kampuni za
Japan zina mipango ya kuwekeza katika kilimo, na hasa kilimo cha pamba
na kuanzisha viwanda vya nguo hapahapa nchini.
Motegi alisema mikakakati mingine ya kuisaidia
Tanzania ni pamoja na kushiriki uboreshaji wa Reli ya Kati, kusaidia
kupanua na kuboresha Bandari ya Dar Es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, mkakati huo wa Japan unatokana na ziara ya Rais Kikwete nchini humo, Juni mwaka huu.
“Japan imeamua kuanzisha ushirikiano mkubwa zaidi
na Tanzania ambako nchi hiyo itaifanya Tanzania kuwa nchi lengwa ya
kuwekeza na kuifanya kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika
Afrika,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliweka wazi kuwa Waziri Motegi
alimweleza Rais Kikwete kuwa ametumwa na Waziri Mkuu Abe, kufuatilia
mazungumzo kati yao na kutangaza rasmi kuwa Japan imeiteua Tanzania kuwa
nchi lengwa na kitovu cha uwekezaji Afrika Mashariki na Afrika kwa
jumla.
Waziri Motegi amesema kuwa katika kufanikisha
mkakati huo aliandamana na kundi la wafanyabiashara wa Japan ambao
wanaendelea kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Tanzania, kuona
jinsi gani wanavyoweza kusaidiana katika kuwekeza katika uchumi wa
Tanzania.
0 comments:
Chapisha Maoni