Ijumaa, Machi 10, 2017

TAARIFA YA ILIYOTOLEWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LEO MACHI 10, 2017

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Kufuatia mapambano yanayoendelea nchi nzima dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na uuzaji na utumiaji wa Pombe kali zilizopigwa marufuku [viroba], Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya misako na Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-

KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.

Mnamo tarehe 09.03.2017 majira ya saa 21:00 usiku Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa wa TANAPA lilifanya msako wa pamoja huko katika Kijiji na Kata ya Lupatingatinga, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watu watatu wakiwa na nyara za serikali.

Watuhumiwa waliokamatwa ni 1. HUSSEIN KHAMIS [33] 2. ISSA MLAWI [31] na 3. ZACHARIA MUSA [36] wote wakazi wa Kijiji cha Matwiga. Watuhumiwa walikamatwa na nyara za Serikali ambazo ni vipande 9 vya meno ya tembo na mikia 2 ya twiga. Watuhumiwa ni majangili. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani.

KUPATIKANA NA POMBE KALI ZILIZOPIGWA MARUFUKU [VIROBA].

Kufuatia msako mkali uliofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa [TFDA] dhidi ya wafanyabiashara wa Pombe Kali zilizopigwa marufuku nchini [viroba] limefanikiwa kuwakamata wafanyabiashara wawili ambao ni ERASMO DANDA [50] Mfanyabiashara na Mkazi wa Ihanga Wilaya ya Mbarali ambaye alikamatwa akiwa na pombe kali zilizopigwa marufuku na serikali aina ya “viroba original” boksi 99 zenye thamani ya Tshs 9,768,000/= zikiwa zimehifadhiwa katika stoo yake. 

Mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa ni JOYCE BATHLOMEO [36] Mfanyabiashara na Mkazi wa Kibaoni Wilayani Chunya akiwa na pombe kali zilizopigwa marufuku na serikali  viroba vya aina mbalimbali ambazo ni “high life”  paketi 180 na aina ya Fiesta paketi 450 zikiwa zinauzwa katika duka lake la jumla.

3. NESTORY FILBERT [23] Mfanyabiashara na mkazi wa Lupatingatinga Wilaya ya Chunya alikamatwa akiwa pombe kali [viroba] paketi 9,840 aina ya Shujaa na paketi 100 za Konyagi.
4. FILBERT KALUMANZILA [60] Mfanyabiashara na mkazi wa Makongolosi Wilaya ya Chunya akiwa na pombe kali [viroba] paketi 240 aina ya ridder.
5. JOSHUA MWAKAJA [42] Mfanyabiashara na mkazi wa Makongolosi akiwa na pombe kali [viroba] paketi 100 aina ya ridder na gun 165 na chupa za ridder 60.
6. JACKSON ELIAS [55] Mfanyabiashara na mkazi wa Makongolosi Wilaya ya Chunya akiwa na pombe kali [viroba] paketi 225 aina mbalimbali.

Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.


KUPATIKANA NA VIPODOZI VILIVYOPIGWA MARUFUKU NA SERIKALI.

Mnamo tarehe 06.03.2017 majira ya saa 13:00 mchana Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako kwa kushirikiana na maafisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tawi la Mbeya [TFDA] katika eneo la Rujewa lililopo Kata na Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata mfanyabiashara mmoja aliyefahamika kwa jina la ASUNGUKYENI MBILINYI [45] Mkazi wa Rujewa akiwa na vipodozi vilivyopigwa marufuku na Serikali aina mbalimbali.

Vipodozi vilivyokamatwa katika msako huo ni betasol lotion tube chupa 240, betasol cream chupa 144, Epiederm cream tube 12, diproson cream tube 12, carlolight cream chupa 8, cocopup chupa 20 na citrolight chupa 6. 

Jumla ya thamani ya bidhaa yote iliyokamatwa ni Tshs. 1,380,000/=. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.


WITO:


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wahalifu na mtandao wa wahalifu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili wakamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kufanya kazi na kuacha kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu kwa ujumla kwani Jeshi la Polisi halitavumilia aina yoyote ya uhalifu. 

0 comments:

Chapisha Maoni