Jumapili, Machi 05, 2017

RIPOTI YA KWANZA YA OPERESHENI MAALUM YA VIROBA

SERIKALI kupitia Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, imesema kupitia kikosi-kazi cha kitaifa cha oparesheni maalum ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali kudhibiti vifungashio vya plastiki vya pombe kali (viroba) iliyoanza jijini Dar es Salaam, Machi Mosi hadi 3 mwaka huu, imekamata chupa zenye ujazo wa mililita 100 ambazo ni 10,625 zenye thamani ya Bilioni 10.83.
Pia bidhaa za pombe kali zilizofungashwa katika viroba vyenye ujazo mdogo zenye thamani ya takribani bilioni 10.8 zimekamatwa na kuzuiliwa katika stoo za viwanda , maduka ya jumla, baa na maghala ya wasambazaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Makamba amesema jumla ya katoni 99,171 za pombe kali za kwenye viroba zilizokamatwa, kati yake vyenye ujazo wa milimita 50 ni katoni 69,045 na milimita 100 ni katoni 29,344, za milimita 90 ni 782 ambapo chupa zenye ujazo wa mililita 100 ni 10,625 zenye thamani ya bilioni 10.83.
Aidha alisema kuwa viroba vyote vilivyokamatwa pamoja na mizigo mingine itabaki chini ya ulinzi kwa sheria zilizotumika na mtu yeyote haruhusiwi kufanya chochote hadi maelekezo zaidi yatakapotolewa na serikali.
Miongoni mwa vikosi-kazi vilivyoshiriki katika oparesheni hiyo ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Ofisi ya Rais (TAMISEMI); Ofisi ya Waziri Mkuu; Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC); Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA); Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na idara zingine za serikali.
“Jumla ya wakaguzi 58 walishiriki katika zoezi hili na kugawanywa katika timu tatu kulingana na mikoa ya kikodi ya TRA Dar es Salaam, ambayo ni Temeke, Kinondoni na Ilala, wakati TFDA na TBS waliainisha viwanda vinavyozalisha pombe kali. Manispaa nazo ziliainisha maduka, maghala na baa zinazofanya biashara ya pombe kali kinyume na sheria,” 
alisema.

0 comments:

Chapisha Maoni