Jumatano, Aprili 06, 2016

RAIS ZUMA ANUSURIKA KUTOLEWA MADARAKANI

Bunge la Afrika Kusini limepinga kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.
Taarifa kutoka Pretoria Afrika Kusini zinaeleza kuwa, bunge la Afrika Kusini limepinga ombi la wabunge wa upinzani waliotaka Rais Zuma apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye. Ombi hilo lilijadiliwa baada ya Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini kumtuhumu Rais wa Afrika Kusini kuwa amekiuka katiba.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Lechesa Tsenoli Naibu Spika wa bunge la Afrika Kusini alitangaza Jumanne wikii hii kuwa mpango wa kumpigia Rais Zuma kura ya kutokuwa na imani umeshindwa kuidhinishwa kwa kura nyingi za wabunge baada ya wabunge wa Afrika Kusini kupiga kura 233 za hapana na kura 143 za ndio.
Hii ni katika hali ambayo Congresi ya Taifa ya Afrika Kusini yaani chama tawala ambacho kinamuunga mkono rasmi Rais Jacob Zuma kimestafidi na wingi wa viti ilivyonavyo bungeni kutokana na theluthi mbili ya kura za hapana zilizopigwa na hivyo kuzuia kura hiyo ya kutokuwa na imani dhidi ya Rais Zuma.
Chama cha Democratic Alliance kiliwasilisha mpango wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani Rais Jacob Zuma kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Katiba wiki iliyopita.
Hata kama Zuma tangu huko nyuma anatuhumiwa kwa ufisadi wa fedha za umma huku Afrika Kusini pia ikiwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ufisadi wa fedha, lakini makelele ya hivi sasa yalianza mara baada ya mahakama ya katiba ya Afrika Kusini kueleza kuwa, Jacob Zuma amekiuka katiba ya nchi hiyo kwa kukataa kurejesha dola milioni 16 fedha za serikali alizotumia kukarabati nyumba yake binafsi.
Mahakama kuu ya Afrika Kusini Alhamisi iliyopita ilitangaza kuwa Rais Zuma ameshindwa kutekeleza na kulinda katiba ya nchi hiyo. Rais Zuma amesema atarejesha serikalini fedha hizo alizotumia kwa matumizi binafsi. Zuma ametamka wazi kuwa hakukiuka katiba kwa makusudi.
Rais wa Afrika Kusini vile vile amewaomba radhi wananchi na serikali na kuvitaka pia vyama vyote vya kisiasa nchini kuheshimu katiba.
Mwaka 2014 Jacob Zuma alitumia karibu Rand za Afrika kusini milioni 216 sawa na dola milioni 24 kutoka hazina ya serikali kwa ajili ya kukarabati makazi yake binafsi.
Kufuatia hukumu hiyo ya mahakama, chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini kilitangaza bungeni kuwa, kitafanya kila linalowezekana ili kumuuzulu Rais Zuma iwapo bunge litashindwa kuchukua hatua katika uwanja huo.
Wawakilishi wa chama cha upinzani cha muungano wa upinzani wa Democratic Alliance katika bunge la Afrika Kusini awali walitangaza kuwa wameuweka katika ajenda ya kazi mpango wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na utendaji wa kisiasa wa Rais Zuma.
Mbali na mpango huo, mpango mwingine pia unatarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni kuhusu tuhuma mpya za ufisadi zinazomkabili Rais Zuma.
Kufuatia hukumu ya mahakama ya Afrika Kusini, Ahmed Kathrada mwanaharakati dhidi ya ubaguzi wa rangi na mmoja wa shakhsia waliokuwa karibu wa marehemu Nelson Mandela, rais wa zamani wa Afrika Kusini pia amemuandikia barua Rais Jacob Zuma akimtaka ajiuzulu. Kathrada ameongeza kuwa, kujiuzulu Zuma kutaisaidia serikali kuondokana na mgogoro wa kukabiliwa na upinzani.
Kabla ya hapo, Rais wa Afrika Kusini aliahidi kupambana na ufisadi slakini hadi sasa hajachukua hatua yoyote katika uga huo, huku mgogoro wa kiuchumi unaoikabili nchi hiyo ukizidi kupanuka.

0 comments:

Chapisha Maoni