Jumamosi, Machi 26, 2016

WATU 150 WAMEHAKIKI SILAHA ZAO, WAPO VIONGOZI WASTAAFU, WABUNGE NA WAFANYA BIASHARA

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Diwani Athumani amesema hadi kufikia sasa zaidi ya watu 150 wamejitokeza kuhakiki wa silaha zao, katika hatua ya kutii agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
“Baada ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kufanya uhakiki wa silaha zake hivi karibuni, watu zaidi ya 150 wakiwemo viongozi mbalimbali waliopo Serikalini, Viongozi wastaafu, Mabalozi wa nchi mbalimbali, wafanyabiashara na wabunge wamejitokeza kuhakiki silaha zao, na wengine wameonesha nia ya kufanya hivyo, hata hivyo tusingependa kutaja majina yao kwa sababu za kiusalama” amesema Kamishna wa Polisi Athumani
Athumani amesema kuwa, lengo la kufanya uhakiki wa silaha ni pamoja na kuboresha hali ya usalama na kuwajua watumiaji, kuwatambua tena wamiliki wa silaha pamoja na kuwa wanawatambua isipokuwa zinaweza kutokea sababu mbalimbali zitakazofanya wasiendelee kumiliki silaha hizo ikiwemo vifo na ulemavu na kusema kuwa wangependa kufahamu taarifa za namna hiyo, ameongeza kuwa zoezi hili sasa ni la nchi nzima si kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee kama ilivyokuwa hapo awali.
Aidha, wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam wanaweza kuhakiki silaha zao katika vituo vya Osterbay Polisi, Temeke Chang’ombe Polisi na Ilala central Polisi, ambapo wanatakiwa kwenda na kitabu(firearm licence book), picha ndogo nne za mhusika, pamoja na anwani sahihi ya mahali anapoishi mhusika.
Vilevile, amewataka viongozi mbalimbali na wananchi wanaomiliki silaha kujitokeza kwa ajili ya kufanya uhakiki wa silaha zao huku akisisitiza kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es salaam, wanaweza kuonana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Simon Sirro na kwa wakazi wa Mikoani waonanae na makamanda wa polisi wa Mikoa yao kwa ajili ya kupewa msaada na maelekezo zaidi ya taratibu za kufuata ili waweze kufanya uhakiki wa silaha zao.

0 comments:

Chapisha Maoni