Vyama vitano vya siasa vitashiriki katika uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, utakaofanyika Machi 20 mwaka huu, uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ADC, CCK, TLP na SAU.
Hatua hiyo inatokana na vyama vitatu vya siasa Zanzibar vya CCK, SAU na TLP, kutangaza kuwa wagombea wake, watashiriki katika uchaguzi huo wa Machi 20. Taarifa ya viongozi wa vyama vya CCK, SAU na TLP, iliyosomwa kwa pamoja katika Ukumbi wa Culture eneo la Mji Mkongwe jana, ilisema wagombea wa vyama hivyo vitatu, watashiriki uchaguzi huo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ulifutwa baada ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali, zilizoonesha wazi kwamba hauwezi tena kuwa huru na haki.
Wagombea wa vyama hivyo vya siasa, waliotangaza kushiriki katika uchaguzi huo ni Ali Khatib kutoka CCK, Issa Mohamed Zonga kutoka SAU na Hafidh Hassan Simai kutoka TLP.
Mgombea wa CCK, Ali Khatib Ali alisema kwamba tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi huo na kuwataka wanachama na wafuasi wake na wananchi, kuitumia fursa hiyo ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaoongoza nchi.
0 comments:
Chapisha Maoni