Ripoti ya siri kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inaituhumu Rwanda kuwa inawasajili na kuwapa mafunzo wakimbizi wa Burundi kwa shabaha ya kumuondoa madarakani Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa na wataalamu waliosimamia vikwazo vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inajumuisha pia ushahidi muhimu unaoonyesha kuwa, Rwanda inaingilia masuala ya Burundi na hivyo kuibua hofu ya kushtadi machafuko ya kisiasa ambayo yanaweza kusababisha umwagaji damu mkubwa.
Ripoti hiyo imeashiria ushahidi uliotolewa na waasi kadhaa ambao waliwaeleza wasimamizi wa vikwazo wa Umoja wa Mataifa kuwa mafunzo hayo yalipewa katika kambi ya wakimbizi ya Mahama iliyoko msituni mashariki mwa Rwanda.
Wataalamu hao wamesema katika ripoti hiyo kuwa walizungumza na waasi 18 wa Burundi katika mkoa wa Kivu Kusini huko mashariki mwa Kongo.
0 comments:
Chapisha Maoni