Jumatatu, Februari 15, 2016

TAARIFA KUTOKA WIZARA YA AFYA KUHUSU UGONJWA WA KIPINDUPINDU

Kama tulivyoahidi Wizara yangu itaendelea kutoa taarifa kila wiki kuhusu ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini. Hadi kufikia tarehe 14 Februari 2016, jumla ya watu 15,853 wameugua ugonjwa huo, na kati yao watu 243 wamepoteza maisha.
Takwimu za wiki iliyopita zinaonyesha kuwa kuanzia tarehe 8 hadi 15 Februari 2016, idadi ya wagonjwa walioripotiwa wiki hii imeongezeka kutoka 242 ya wiki iliyoishia tarehe 7 February hadi 528 ambapo ni sawa na ongezeko la 118%, kati yao watu 5 walipoteza maisha. Ongezeko hili limechangiwa zaidi na kuibuka tena kwa ugonjwa huu mkoani Iringa katika Halmashauri ya Iringa ambayo imeripoti jumla ya wagonjwa 199 kwa wiki iliyopita ikiwa ni sawa na 38% ya wagonjwa wote walioripotiwa kwa wiki husika. Huko nyuma katika mwezi Julai, Mkoa wa Iringa uliwahi kuripoti wagonjwa 2 kwa siku moja tu, hata hivyo wagonjwa hao waliripotiwa katika halmashauri tofauti za Mufindi (1) na Iringa Mjini (1). Mkoa wa Dar Es Salaam ambapo ugonjwa ulidumu sana kwa muda wa miezi 4 na baadae kutoweka kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa umeanza tena kuripoti wagonjwa. Katika wiki iliyopita mkoani Dar es salaam waliripotiwa wagonjwa 6 ambao walitokea Manispaa ya Temeke. Jumla ya mikoa ambayo imeripoti kuwa na wagonjwa kwa wiki iliyopita ni 11 ikiongozwa na Iringa 199 (Halmashauri ya Iringa Vijijini 199) ikifuatiwa na Mkoa wa Mwanza 87 (Ilemela 31, Ukerewe 26, Nyamagana 15, Buchosya 11 na Sengerema 4), Mara 84 (Musoma mjini 36, Tarime vijijini 17, Musoma Vijijini 12, Butiama 10, Tarime Mjini 5 na Rorya 1). Mikoa mingine ni pamoja na Morogoro 54, Arusha 49, Simiyu 16, Dodoma 11, Mbeya 8, Kilimanjaro 8, Dar es salaam 6 na Manyara 6.
Katika kudhibiti ugonjwa huu Wizara imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na mwitikio mdogo wa jamii katika kudhibiti ugonjwa hasa kwenye suala la usafi wa mazingira na vyoo, pamoja utumiaji wa maji safi na salama. Hii ni pamoja na kufuata sheria ndogo ndogo zilizowekwa na jamii husika katika kuhakikisha suala zima la usafi. Vilevile uelewa mdogo wa jamii kuhusu sababu zinazochangia kuwepo kwa ugonjwa wa kipindupindu pamoja na mila potofu zimekuwa ni changamoto katika swala zima la kumaliza ugonjwa huu, kama ilivyodhihirishwa huko Kyela mkoani Mbeya ambako mila potofu zimehusishwa na sababu za ugonjwa wa kipindupindu na kusababisha vifo kwa watu wasiokuwa na hatia. Wizara inasisitiza kwa mikoa na halmashauri zote kutilia mkazo suala la uelimishaji jamii kwa kushirikisha viongozi mbalimbali ikiwa pamoja na ushirikishwaji wa walimu wa shule, viongozi wa dini, kimila na viongozi wengine wanaokubalika na jamii husika katika kuelimisha na haswa swala la mila potofu.
Wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti ugonjwa ikiwa ni pamoja na kupeleka timu mbalimbali kutoka ngazi ya taifa katika mikoa ambayo bado kuna changamoto ikiwa ni pamoja na Morogoro, Simiyu, Mwanza, Mara, Mbeya na Manyara ili kuweza kushirikiana na mikoa hiyo katika kudhibiti Ugonjwa wa Kipindupindu. Vilevile kutokana na ongezeko la wagonjwa katika Halmashauri ya Iringa Wizara imetuma timu ya wataalamu kushirikiana na timu za mkoa na Halmashauri katika shughuli za kudhibiti ugonjwa huu. Aidha Wizara ilikwishapeleka dawa na vifaa tiba na juhudi za kupata dawa na vifaa zaidi zinaendelea. Bado naendelea kusisitiza mapambano ya Kipindupindu yanahitaji ushirikishwaji wa ngazi zote mpaka katika ngazi ya kaya hivyo tukishirikiana kwa pamoja tutatokomeza Kipindupindu. Kutokana na uzoefu kutoka mikoa ya Dar Es Salaam na Iringa kutoweka na kurudi tena kwa ugonjwa huu, na pia kutokana na ukweli kuwa ugonjwa upo pia katika nchi za jirani, Wizara inasisitiza Mikoa na Wilaya kuendelea kuimarisha mikakati ya kuzuia wa kipindupindu na kuifanya kuwa endelevu.
Hitimisho
Wizara inaendelea kutoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kila mmoja kutimiza wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.
Kwa mara nyingine tena tunaendelea kuwashukuru wadau wote, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada zetu za kupambana na magonjwa.

0 comments:

Chapisha Maoni