Jumatatu, Februari 01, 2016

TAARIFA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA ZIKA (ZIKA VIRUS)

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAARIFA KWA WANANCHI NA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA ZIKA (ZIKA VIRUS)
1. Utangulizi
Kumekuwepo na taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya Kitaifa na Kimataifa kuhusu Homa ya Zika ambao ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus”. Ugonjwa huu uligundulika kwa mara ya kwanza nchini Uganda katika miaka ya 1947 kwenye wanyama aina ya sokwe/nyani (rhesus macaque) ndani ya Misitu ya Zika, karibu na Ziwa Victoria. Mnamo mwaka 1952, ugonjwa wa zika uligundulika kwa binadamu nchini Uganda na Tanzania, na mwaka 1968 uligunduliwa nchini Nigeria. Kuanzia mwaka 1951 hadi 1981, ugonjwa huu umeshatolewa taarifa katika nchi takribani sita (6) za Afrika ambazo ni Afrika ya Kati, Misri, Gabon, Sierra Leone, Tanzania na Uganda. Vile vile, ugonjwa huu umeshatolewa taarifa katika nchi za India, Indonesia, Malaysia, Philipine, Thailand na Vietnam na pia nchi za Amerika na Pacific.
Kuanzia mwezi Mei 2015, ugonjwa huu ulianza kutolewa taarifa ambapo hadi sasa umeathiri zaidi Bara la Amerika ya Kusini. Kuna takribani nchi 22 ambapo Wagonjwa wamethibitishwa kimaabara kuwa na ugonjwa wa Zika. Nchi hizo ni Brazil (Majimbo 14 yameathirika), Colombia, Suriname, El Salvador, Guatemala, Paraguay, Mexico, Venezuela, Panama, Cape Verde, Honduras, Panama, France (French Guiana na Martinique, United States of America (Puerto Rico), Guyana, Barbados, Ecuador, Bolivia, Haiti, Ujerumani, France (Saint Martin and Guadeloupe na Dominican Republic.
Ugonjwa huu unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye (huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana/jioni). Aina hii ya kirusi ipo katika familia ya “Flavirus” ambapo pia wapo virusi vya ugonjwa wa Dengue, Homa ya Manjano (Yellow Fever), Japanese ancephalitis na West Nile Virus.
Kirusi cha homa ya Zika kama kile cha Dengue kinaambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu wa jamii ya Aedes hasa Aedes aegypti. Mbu huyu anaishi katika mazingira ya makazi ya binadamu, huuma wakati wa mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususani majira ya asubuhi na jioni kabla ya jua halijazama. Mbu huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari, ndoo, makopo nk.
2. Dalili za Homa ya Zika
Dalili za ugonjwa huu zinafanana na za homa ya Dengue, ambazo ni homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya viungo, macho kuwa mekundu na vile vile kupata vipele vidogo vidogo kama harara (Skin rashes). Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 2 hadi 7 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya Zika.
Uko uwezekano, ambao haujathibitishwa rasmi, kwamba wakati mwingine wagonjwa wanaweza kupata matatizo katika ubongo (Neurological Complications) na miguu kupooza (Gullein Barre Syndrome), na wajawazito huweza kujifungua watoto wenye ulemavu wa kichwa yaani kichwa kuwa kidogo kulingana na umri wa mtoto (microcephaly).
Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria. Hivyo basi, natoa rai kwa wananchi kuwa, wakati wanapojisikia homa au wamepata homa wahakikishe wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria au la, kwa kuwa dalili za ugonjwa wa Zika zinaweza kufanana sana na dalili za malaria.
Homa ya Zika inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka. Hakuna dawa maalum ya ugonjwa huu wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji na damu.
3. Ugonjwa wa Homa ya Zika haujaingia Tanzania
Mara tu baada ya kuwepo kwa taarifa juu ya ugonjwa huu, Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini pamoja na mipakani kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa (surveillance system ya Wizara).
Tumejiridhisha kuwa ugonjwa wa homa ya Zika kwa sasa haujaingia nchini kwetu. Hivyo, Wananchi wasiwe na hofu ila waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu pamoja na magonjwa ya Dengue na Malaria kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuzingatia yafuatayo:-
(i) Kuangamiza mazalio ya mbu kwa:
kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyizia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo.
kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile; vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk. 
kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu.
Kuhakikisha kuwa maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama.
kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara.
kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.
(ii) Kujikinga na kuumwa na mbu kwa;-
Kutumia viuatilifu vya kufukuza mbu “mosquito repellants”.
Kuvaa nguo ndefu ili kujikinga na kuumwa na mbu.
Kutumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala majira ya mchana hasa watoto).
kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi.
4. Hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ni pamoja na:-
Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inaendelea kuwasiliana na kushirikiana kwa karibu na Shirika la afya Duniani – Ofisi ya Tanzania kwa lengo la kupata Taarifa na maelezo zaidi ya kukabiliana na ugonjwa huu. Kamati ya Dharura ya Miongozo ya Kimataifa ya Afya ya WHO yaani “International Health Regulations Emergency Committee” itakutana siku ya Jumatatu ya tarehe 1/2/2016, mjini Geneva,Uswisi ili kufanya tathmini ya ugonjwa huo na kutoa tamko na maelekezo zaidi ya namna ya kudhibiti Ugonjwa huu kwa nchi wanachama.
Baada ya tamko/Mwongozo huo wa WHO, Wizara ya Afya itaandaa Taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kwa ajili ya kusambazwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya Tanzania Bara. Aidha, taarifa hii itajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (ainisho la Ugonjwa), “Ukweli Kuhusu Ugonjwa” (Fact Sheet), Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu vitatolewa.
Wizara itaanza kutoa elimu kwa wananchi kupitia Radio na Runinga kuhusu ugonjwa huu sambamba pia na ugonjwa wa Dengue ambao uambukizi wake unasababishwa na Mbu aina ya Aedes.
Kuendelea kutoa vyandarua vyenye uatilifu katika Mkoa yote Tanzania ili kufikia lengo la asilimia 95.
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na mipakani kupitia mfumo wa surveillance ya Wizara. Aidha, Wizara inatoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya hapa nchini kutoa taarifa za watoto watakaozaliwa wakiwa na ulemavu wowote wa kichwa ikiwemo “microcephaly” au “anencephaly”.
Kufuatilia kwa karibu ongezeko la wagonjwa wenye homa isiyokuwa ya malaria kwa Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi wa kina iwapo kuna ugonjwa huu.
Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina kupitia maabara ya Taifa iliyopo katika Taasisi ya uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (Centre for Disease Control (CDC) katika kuhakikisha kuwa vitendanishi vya kutambua ugonjwa huu vinapatikana.
Kushirikisha program ya Malaria na NIMR katika kudhibiti mbu kwa kupulizia na kunyunyizia viuatilifu. Hii inalenga kuangamiza mbu wapevu na viluwiluwi.
5. Hitimisho
Ugonjwa wa Homa ya Zika bado haujaingia Tanzania. Wananchi waondoe hofu juu ya uwepo wa ugonjwa huu. Hata hivyo, ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya Zika, Dengue na malaria ambayo huenezwa kwa namna inayofanana.
Aidha, mvua hizi kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini zinaweza kuchangia kuongezeka kwa mazalio ya mbu. Hivyo, utupaji, uzoaji na uhifadhi wa taka katika vijiji na miji yetu ni lazima uimarishwe katika kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa salama kwani bila ya kuzingatia hayo, tunatoa fursa kwa mazalio ya mbu kuongezeka na hata kuwa karibu zaidi ya makazi ya binadamu.
Wizara ya Afya itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi ili waweze kuelewa kuhusu ugonjwa huu na kuchukua hatua stahiki.
Imetolewa na:-
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
31/1/2016

0 comments:

Chapisha Maoni