Jumatatu, Februari 01, 2016

SHEIN: CCM TUTASHIRIKI UCHAGUZI; WALIOSUSIA SHAURI YAO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amesema kuwa, chama hicho kipo tayari kwa uchaguzi wa marudio hapo Machi 20 kwa lengo la kuhakikisha kinashika dola na waliochukua uamuzi wa kususa ni maamuzi yao binafsi.
Dakta Muhamed Shein amesema suala la chama cha siasa kushiriki au kutoshiriki ni jambo la hiyari katika misingi ya demokrasia. Amesema, uchaguzi Mkuu wa marudio Zanzibar haukuitishwa na CCM, CUF au Chadema, bali Tume ya Uchaguzi ndio walioitisha baada ya kujiridhisha kuwa Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana ulikuwa na kasoro. Rais wa Zanzibar amesema Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad ndiye aliyekiuka makubaliano ya mazungumzo ya mwafaka na kukimbilia katika vyombo vya habari. Dakta Shein amesema kuwa, amesikitishwa na uamuzi pamoja na kauli za Katibu Mkuu wa CUF ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad za kujitoa katika mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika, ambayo wote kwa jumla walikubaliana kwamba yawe siri kwa muda wote.
Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia katika mgogoro wa kisiasa miezi Oktoba mwaka jana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichokiita ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa zoezi la upigaji kura.


0 comments:

Chapisha Maoni