Rais wa Sudan Kusini amemteua hasimu wake mkubwa wa kisiasa Riek Machar kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Televisheni ya taifa ya Sudan Kusini imesema kuwa, Rais Salva Kiir amemteua Riek Machar kuwa Makamu wa Rais ikiwa ni sehemu ya mpango wa amani wenye lengo la kuhitimisha vita vya ndani vya zaidi ya miaka miwili sasa.
Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilianza Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu Riek Machar aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo kwamba, alipanga njama za kuipindua serikali. Sudan Kusini ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu wakati huo huku raia wasio na hatia wakiuawa na wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kuwa wakimbizi.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zimekuwa zikizituhumu pande zote mbili huko Sudan Kusini kwamba, zimetenda jinai dhidi ya binadamu.
Kuteuliwa Machar kuwa Makamu wa Rais kumehuisha tena matumaini ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo kwa mujibu wa makubaliano ya amani yalitotiwa saini na pande husika Agosti mwaka jana. Matumaini hayo yalikuwa yamefifia hivi karibuni baada ya kutolewa taarifa za kuvunjika makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni