Jumatatu, Februari 01, 2016

RIPOTI YA FICHUO KUHUSU MICHUANO YA CHAN

Nchi 8 zimetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kuwania ubingwa wa soka barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza barani humo CHAN, katika kindumbwendumbwe kinachoendelea kurindima nchini Rwanda. Wenyeji Rwanda wamelazimika kuyaaga mashindano hayo baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mchuano wa robo fainali uliopigwa katika uwanja uliokuwa umefurika mashabiki zaidi ya 30,000 wa Amahoro jijini Kigali wikendi hii. DRC ndio waliokuwa wa kwanza kucheka na nyavu za Rwanda kupitia bao la Doxa Gikanji dakika 10 baada ya kuanza mchezo.

Hata hivyo Rwanda walirekebisha kasoro zilizojitokeza katika kipindi cha kwanza, na kulipiza bao hilo kupitia mchezaji Earnest Sugira dakika 11 baada ya kutoka mapumzikoni. Ilibidi timu hizo ziongezewe dakika 30 baada ya dakika 90 za ada kumalizika kwa sare hiyo ya 1-1, na hapo ndipo kitumbua cha mwenyeji Rwanda kikaingia mchanga baada ya Bompunga kuipa DRC bao la ushindi katika dakika ya 113 na kujikatia tiketi ya nusufainali. Kichapo hicho kilikua pigo jingine kwa soka ya Rwanda, haswa ikizingatiwa kuwa vijana hao wa Amavubi walishindwa kufurukuta mbele ya Uganda katika mchuano wa fainali wa Cecafa mwishoni mwa mwaka jana 2015. Huku hayo yakiripotiwa, Kodivaa pia imejikatia tiketi ya nusu fainali ya CHAN baada ya kuisasambua Cameroon mabao 3-0 katika mchuano mwingine wa robo fainali Jumamosi hii. Mabao yote 3 yalifugwa katika muda wa nyongeza, baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika bila timu hizo kufungana. Mabao ya Ivory Coast yalifungwa na Koffi Boua (95), Atcho Djobo (dakika 7 baadaye) na Serge N’Guessan dakika 112.
Kwengineko, mlinda lango wa timu ya mpira wa miguu wa Guinea Abdul Aziz Keita, aliwastaajabisha wengi baada ya kufunga mkwaju wa penalti dhidi ya Zambia katika mchezo mwingine wa robo fainali na hivyo kuikatia timu yake tiketi ya nusu fainali ya michuano hiyo. Katika mchuano huo wa Jumapili, timu hizo zilimaliza dakika 90 bila kufungana na pia kushindwa kuona lango la kila mmoja katika dakika 30 za ziada na hivyo mchuano huo kulazimika kuamuliwa ma mikwaju ya penati. Wakati huo huo, Tunisia ambayo imewahi kutwaa taji hilo imeshindwa kusonga mbele baada ya kulazwa mabao 2-1 na Mali na sasa watakabana koo na Kodivaa katika mchuano wa nusu fainali kati kati ya wiki hii. Mabao ya Mali yalifungwa na Aliou Dieng na Abdoulaye Diarra. Hadi sasa Ahmed Akaichi kutoka Tunisia anaongoza katika safu ya ufungaji mabao kwa kutikisa nyavu mara 4, sawa na Chisom Chikatara kutoka Nigeria ambayo imeaga michuano hii.

0 comments:

Chapisha Maoni