Jumatatu, Februari 08, 2016

MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI NA TAHADHARI YA UGONJWA WA HOMA YA ZIKA

Kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, huu ni mwendelezo wa taarifa ya wiki kwa umma, ya mwenendo wa ugonjwa huu hapa nchini. Hadi kufikia tarehe 7 Februari 2016, jumla ya watu 15325 wameugua ugonjwa huo, na kati yao watu 238 wamepoteza maisha kwa ugonjwa huu.
Takwimu za Kuanzia tarehe 1 hadi 7
Februari 2016, zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa walioripotiwa wiki hii imepungua kutoka 459 ya wiki iliyoishia tarehe 31 Januari hadi 258 ambapo ni sawa na punguzo la asilimia 44. Kuna vifo 5, sawa na idadi ya vifo vilivyoripotiwa katika wiki iliyopita.
Jumla ya mikoa ambayo imeripoti kuwa na wagonjwa ni 13 ambapo mkoa wa Mara ndio umeongoza kwa kuripoti idadi kubwa zaidi ya wagonjwa ukilinganishwa na mikoa mingine, ukiwa na wagonjwa 73 (Musoma Vijijini 33, Musoma mjini 5, Bunda 1, Butiama 13, na Tarime Vijijini 21), ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza (70)- (Ukerewe 21, Nyamagana 24, Ilemela 8, Sengerema 5 na Buchosa 12). Mikoa mingine ni pamoja na Simiyu (30), Morogoro (26) na Kilimanjaro (16).
Katika mapambano ya kudhibiti mlipuko huu wa Kipindupindu, kuna changamoto mbalimbali zilizobainishwa na Wizara yangu kupitia wataalam ambao wanashirikiana na timu zilizopo katika mikoa na wilaya zilizoathirika. Mojawapo wa changamoto ni utoaji wa idadi pungufu ya wagonjwa au kutotoa kabisa taarifa za wagonjwa wa Kipindupindu. Hii inapelekea kusababisha mikakati iliyowekwa kutokuwa na mafanikio hivyo ugonjwa kuendelea kuwa ni tishio katika jamii. Ninapenda kusisitiza kuwa, taarifa za wagonjwa wa Kipindupindu zitolewe bila kuficha, na watendaji watakaoficha taarifa za wagonjwa watawajibishwa ipasavyo.
Changamoto nyingine iliyopo ni ushiriki mdogo wa sekta nyingine katika kupambana na ugonjwa huu. Ninaomba ieleweke kuwa mapambano dhidi ya Kipindupindu yatafanikiwa ikiwa sekta nyingine kama Maji, miundombinu, biashara, elimu, mazingira n.k zitashirikiana. Wizara yangu imeendelea kusisitiiza ushirikiano huu katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya, ili mipango ya kupambana na Kipindupindu ishirikishe sekta mbalimbali na pia Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za Dini na Vyombo ya Habari.
Wizara imeendelea kupeleka timu mbalimbali kutoka ngazi ya taifa katika mikoa ambayo bado kuna changamoto ikiwa ni pamoja na Morogoro, Simiyu, Mwanza, Mara, Mbeya na Manyara ili kuweza kushirikiana na mikoa hiyo katika kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu. Bado naendelea kusisitiza mapambano ya Kipindupindu yanahitaji ushirikishwaji wa ngazi zote hadi katika ngazi ya kaya hivyo tukishirikiana kwa pamoja tutatokomeza Kipindupindu
Ndugu Waandishi wa Habari,
Pamoja na mapambano dhidi ya Kipindupindu, Wizara yangu inaendelea kutoa tahadhari ya Ugonjwa wa Homa ya Zika, unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus”.
Ugonjwa wa Homa ya Zika unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana au jioni. Aina hii ya kirusi ipo katika familia ya “Flavivirus” ambapo pia vipo virusi vya ugonjwa wa Dengue, Homa ya Manjano (Yellow Fever) na wengineo.
Kuanzia mwezi Mei 2015, ugonjwa huu ulianza kutolewa taarifa ambapo hadi sasa umeathiri zaidi Bara la Amerika ya Kusini.
Kuna takriban nchi 22 ambako wagonjwa wamethibitishwa kimaabara kuwa na ugonjwa wa Zika. Mlipuko wa ugonjwa huu umethibitishwa na Shirika la Afya Duniani kuwa ni janga la kimataifa. Napenda kusema kuwa hakuna mgonjwa yeyote ambaye amekwisharipotiwa nchini Tanzania hadi sasa.
Hata hivyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na kuwatoa hofu wananchi, inawakumbusha kuwa waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Zika pamoja na magonjwa mengine yanayoenezwa na mbu ikiwa ni pamoja na kuzingatia yafuatayo:-
(i) Kuangamiza mazalio ya mbu kwa:
kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyizia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo.
kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile; vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu.
Kuhakikisha kuwa maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama.
kufunika mashimo ya maji taka kwa mifuniko imara.
kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.
(ii) Kujikinga na kuumwa na mbu kwa;-
Kutumia viuatilifu vya kufukuza mbu “mosquito repellants”.
Kuvaa nguo ndefu ili kujikinga na kuumwa na mbu.
Kutumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala majira ya mchana hasa watoto).
kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi.
Serikali, kupitia Wizara yangu pamoja na wadau inaendelea kusimamia yafuatayo:
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na mipakani kupitia mfumo wa ufuatiliaji magonjwa “surveillance” ya Wizara.
Aidha, kufuatilia kwa karibu ongezeko la wagonjwa wenye homa isiyokuwa ya malaria kwa Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi wa kina iwapo kuna ugonjwa huu.
Kuendelea na mikakati ya kudhibiti mbu waenezao magonjwa ikiwa ni pamoja na kusistiza matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu
Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina kupitia maabara ya Taifa iliyopo katika Taasisi ya uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (Centre for Disease Control (CDC) katika kuhakikisha kuwa vitendanishi vya kutambua ugonjwa huu vinapatikana.
Kushirikisha program ya Malaria na NIMR katika kudhibiti mbu kwa kupulizia na kunyunyizia viuatilifu. Hii inalenga kuangamiza mbu wapevu na viluwiluwi.
Kuhakikisha utoaji wa tiba sahihi na kwa wakati
Wizara itaanza kutoa elimu kwa wananchi kupitia Radio na Runinga kuhusu ugonjwa huu sambamba pia na ugonjwa wa Dengue ambao uambukizi wake unasababishwa na Mbu aina ya Aedes.
Kufuatilia wajawazito kwa ajili ya kupata taarifa za watoto watakaozaliwa wakiwa na ulemavu wowote wa kichwa ikiwemo “microcephaly” au “anencephaly”.
Hitimisho
Wizara itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi ili waweze kuelewa kuhusu magonjwa haya pamoja na ugonjwa wa Zika na kuchukua hatua stahiki. Aidha, ninatoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kila mmoja kutimiza wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu na tahadhari ya Ugonjwa wa Zika.
Tunawashukuru wadau wote, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada zetu za kupambana na magonjwa.

0 comments:

Chapisha Maoni