Jumamosi, Februari 13, 2016

ALICHOKIFANYA DKT. KIGWANGALA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA LEO

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dk. Hamisi Kingwangalla amefanya ziara, Februari 12, 2016 katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Nyanda za juu kusini- Mbeya, na kutoa maagizo mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mashine CT-Scan ndani ya siku 60 huku akibainisha kuwa endapo watazembea basi watawachukulia hatua kali na kuwajibishwa watendaji na uongozi wa Hospitali hiyo.
Dk. Kigwangalla alifika hospitalini hapo majira ya saa tisa alasiri na kutembelea idara mbalimbali za hospitali hiyo kuona jinsi ya ufanyaji kazi ambapo ndipo alipobaini ukosefu wa mashine hiyo ya CT-Scan pamoja na vifaa vingine muhimu ambavyo alibainisha kuwa hata uongozi wa Hospitali hiyo walikuwa na uwezo wa kuvinunua bila kutegemea Serikali.
Baadhi ya idara ambazo, Dk. Kingwangalla alitembelea ni pamoja na kitengo cha kutolea huduma kwa wagonjwa (OPD), Kitengo cha upasuaji, wodi ya upasuaji, duka la dawa la hospitali hiyo, wodi ya wanawake, wodi ya wanaume, watoto na kitengo cha Maabara ambapo kisha alipata kuongea na wafanyakazi pamoja na uongozi mzima wa Hospitali.
Dk.Kigwangalla alitoa wasaha mwingi kusikiliza kero za wafanyakazi hao kuongea lile linalowakabili bila kuogopa ili aweze kujua matatizo na changamoto zinazowakabili.
"Hospitali kubwa kama hii hapa Mbeya na wataalam wote mlionao mnashindwa kufanya biashara!, Mnategemea tu Serikali? lini mtakuwa na CT-scan kwa upande wenu? wakati mnaingiza Milioni 500 kwa mwezi?" alihoji Dk. Kigwangalla.
Dk.Kigwangalla aliwaambia uongozi wa hospitali hiyo ina fursa na uwezo wa kufanya jambo kubwa kwani pia ina uwezo hata wa kukopa fedha kutoka mashirika ya bima ya afya.
Aidha, Dk Kigwangalla amewataka uongozi wa Hospitali hiyo kuwa wabunifu katika uendeshaji wao ikiwemo kutengeneza jengo la kisasa la matibabu ya kulipia, kujenga nyumba za wafanyakazi ambapo amewapa mikakati hiyo imeanza na pindi atakaporejea tena hospitali hiyo.
Imeandaliwa na Andrew Chale, modewjiblog, Mbeya

0 comments:

Chapisha Maoni