Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za Maafisa wanaofanya kazi kinyume na maadili.
Akiongea na mwandishi wa habari hii leo Jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Richard Kayombo amesema kuwa TRA ina Idara Maalumu ijulikanayo kama Idara ya Mambo ya Ndani ya TRA ambayo inashughulika na kufuatilia maadili ya watumishi wa sekta hiyo nchi nzima.
“Tunawaomba wananchi kushirikiana na Idara ya Mambo ya Ndani ya TRA kwa kuwapa taarifa juu ya maafisa wa TRA wanaokwenda kinyume na Maadili ya Utumishi wa Umma,”alisema Kayombo.
Mkurugenzi Kayombo ameongeza kuwa wananchi wanaweza kutoa taarifa kwa kupiga simu kwa namba 0689122515 au kwa kutuma ujumbe mfupi kwa simu namba 0689122516 na kuwahakikishia kuwa taarifa zao zitakua zimefika sehemu husika na zitafanyiwa kazi.
Aidha Kayombo amependa kuwatoa wasiwasi wananchi kuwa namba hizo ni za siri na hakuna mwananchi atakayepata tatizo lolote kwa kutoa taarifa za maafisa wasio na maadili.
TRA kupitia Idara yake ya Mambo ya Ndani imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya watumishi wa TRA wanaoenda kinyume na maadili, wameyafanyia uchunguzi na baadhi ya watumishi wamefukuzwa na wengine kupewa adhabu kali.
0 comments:
Chapisha Maoni