Jumatano, Januari 06, 2016

MADAKTARI WA UINGEREZA KUANZA MGOMO WIKI IJAYO

Waziri wa Afya wa Uingereza amesema kuwa, mgomo wa madaktari uliopangwa kufanyika wiki ijayo nchini humo utasababisha hasara na madhara makubwa kwa wagonjwa na kukwaza huduma za afya katika nchi hiyo ya Ulaya.
Jeremy Hunt amekosoa vikali hatua ya madaktari hao ya kuitisha mgomo wiki ijayo ilihali mazungumzo kati yao na serikali yangali yanaendelea. Waziri wa Afya wa Uingereza amesema kama ninavyomnukuu: "Hakukuwa na dharura ya kuitisha mgomo madaktari hao wakati huu wa kuendelea mazungumzo," mwisho wa kunukuu.
Mgomo huo umeitishwa na Jumuiya ya Madktari ya Uingereza kufuatia kile kinachoelezwa na jumuiya hiyo kwamba, ni mkwamo katika mazungumzo kati ya pande mbili.
Jumuiya hiyo imesisitiza kuwa, Jumanne ya wiki ijayo wanachama wake wataanza kufanya mgomo baada ya serikali ya London kushindwa kushughulikia matatizo yao.
Hata hivyo serikali ya Uingereza kupitia waziri wake wa afya inakanusha kukwama mazungumzo hayo na badala yake imeikosoa hatua ya Jumuiya ya Madaktari nchini humo ya kuitisha mgomo na kuitaja kuwa ni ya kukatisha tamaa.
Miongoni mwa matakwa ya madaktari hao ni kuongezwa malipo na mishahara yao.

0 comments:

Chapisha Maoni