Moja ya majukumu ya Wakala wa Ukaguzi wa madini Tanzania (TMAA) ni
kufuatilia na kuzuia utoroshaji/magendo na biashara ya madini
unaopelekea ukwepaji wa ulipaji mrabaha kwa kushirikiana na taasisi
nyingine husika za Serikali zikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA),
Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na Idara ya Uhamiaji.
Taarifa za matukio ya udhibiti wa utoroshaji na biashara haramu
ya madini zilizopo zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi
Julai 2015 mpaka Januari 13, 2016 kulikuwepo na jumla ya matukio 14 ya
utoroshaji wa madini ambapo madini yenye thamani ya Dola za Marekani
1,474,194 milioni (zaidi ya Shilingi bilioni 3,235,856,181) yalikamatwa
na wakaguzi wa Wakala kupitia Madawati ya Ukaguzi yaliyopo katika
viwanja vya ndege vya Dar es Salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Mwanza.
Katika matukio ya hivi
karibuni ya ukamataji wa madini katika viwanja vya ndege, madini yenye
thamani ya jumla ya Shilingi milioni 11,217,300 yalikamatwa na wakaguzi
wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya dola.
Raia mmoja wa kigeni na mwingine wa Tanzania
walikamatwa wakiwa na madini hayo bila kuwa na kibali chochote cha
usafirishaji kulingana na Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Raia wa kigeni
(jina limehifadhiwa) ambaye alikuwa anasafiri kwenda Bangkok alikamatwa
akiwa na madini aina mbalimbali ikiwemo almasi, aquamarine, sapphire,
green tourmaline, quartz na rhodolite.
Tukio la pili, mtuhumiwa
mwingine ambaye ni raia wa Tanzania aliyekuwa akisafiri kwenda Ujerumani
alikamatwa akiwa na madini mbalimbali ikiwemo amethyst, moonstone
cabochon, rulilated quartz (cabochon), rulilated quartz(faceted),
chrysoprase, green tourmaline, ruby, red garnet, green quartz, zircon na
rhodolite.
Kufuatia Matukio hayo wahusika wote wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufunguliwa kesi mahakamani.
Wakala unatoa rai kwa Umma kujiepusha na shughuli za utoroshaji/magendo
na biashara haramu ya madini, kwani hatua kali zitaendelea kuchukuliwa
kwa yeyote atakayebainika/kukamatwa akijihusisha na shughuli hizo.
Aidha, madini yatakayokamatwa yakisafirishwa kinyume cha sheria na
taratibu zilizopo yatatafishwa na Serikali.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini inatoa wito kwa
yeyote atakayetoa taarifa za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya
madini kwa Kamishna wa Madini au Wakala ambazo zitawezesha ukamataji wa
madini, atazawadiwa fedha taslimu ambazo ni sawa na asilimia 5 ya
thamani ya madini yatakayokamatwa na kunadiwa. Kwa mawasiliano ya
haraka, wananchi watumie barua pepe info@tmaa.go.tz na simu 022-2137142
au 022-2601819.
0 comments:
Chapisha Maoni