Jumatano, Januari 13, 2016

KAZI YA KUWAONDOA WAGENI WANAOZIBA FURSA ZA WAZAWA YAPAMBA MOTO TANZANIA

Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Eng. Hamad M.Y. Masauni amesisitiza kuwa Operesheni inayoendeleea sasa nchini kote haina lengo la kuwafukuza nchini wageni wenye vibali halali vya kuishi ama kutembelea chini, bali lengo lake ni kuwasaka na kuwahamisha wageni wote wanoishi nchini kinyume na Sheria ya Uhamiaji Na. 54 ya mwaka 1995. Mhe. Masauni amesisitiza kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi haitorudi nyuma katika kuhakikisha kuwa inasimamia utekelezaji wa sheria za nchi zilizotungwa kwa ajili ya kulinda maslahi ya nchi na wananchi wake kiusalama, kiuchumi na kijamii. Hayo aliyazungumza katika Ofisi kuu ya Uhamiaji Zanzibar iliyopo eneo la Kilimani alipofanya ziara yake ya kikazi ili kujionea shughuli za utendaji za ofisi hiyo. 
“Operesheni hii ni ya kitaifa, imeanza Dar es salaam na kuendelea katika Mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Mikoa yote ya Zanzibar. Hivyo, nawasisitiza kuwasilisha ripoti yenu ya utekelezaji wa zoezi hili ya kila wiki kupitia Makao Makuu ikihusisha pia utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Waziri na Naibu Waziri wakati wa ziara zetu”. Alisisitiza Mhe. Masauni.
Waziri huyo amesema kuwa Serikali chini ya Idara ya Uhamiaji itapambana na wahamiaji waliopo nchini bila vibali ama kufuata kanuni na sheria zinazoruhusu ukaazi wao na si vinginevyo. Hivyo wageni wote wenye vibali vinavyowaruhusu kuwepo nchini hawatobugudhiwa kwa namna yoyote ile. Hata hivyo alionya, maofisa wa Idara ya Uhamiaji kutekeleza zoezi hilo kwa weledi na uadilifu na kwa kufuata misingi ya sheria, utawala bora na haki za binaadamu, na katika kuteleza kazi hiyo, afisa yeyoye atakae bainika kuwanyanyasa au kuwadhalilisha wageni atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
“Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine yoyote duniani tunapenda wageni na hatuwezi kujitenga, tumejenga mahusiano mazuri na mataifa mbali mbali duniani na tumekuwa mstari wa mbele katika kuheshimu mikataba kimataifa na kikanda. Watanzania pia tunasifika kwa ukarimu wetu wa asili kwa wageni. Aidha, tutaendelea kutambua na kuthamini mchango wa wataalamu wa kigeni, watalii na wawekezaji waliopo nchini katika kuinua uchumi wa taifa letu, hivyo hatuwezi kuwafukuza ama kuwabughuzi wageni ambao wako nchini kihalali” 
alisema Eng. Masauni.
Aidha amewataka maafisa wa uhamiaji kutotumia zoezi hilo la kubaini wakaazi haramu kwa manufaa yao na yeyote atakae bainika kutumia zoezi hilo kinyume na agizo la serikali atashughulikiwa kwani serikali haijapanga kuonea wala kunyanyasa mtu yeyote yule.
Naibu huyo aliongeza kuwa sheria zilizopo nchini ni kwa ajili ya manufaa ya nchi na watu wake, hivyo ni lazima kila mtu aziheshimu na kuwa Serikali haina lengo la kutumia sheria hizo kukandamiza wageni, bali ni kulinda maslahi ya nchi yetu kiuchumi na kusalama.
Pamoja na hayo Masauni alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga kutatua kero za wananchi, hivyo Idara ya Uhamiaji iache kufanya kazi kwa mazoea na kwamba iendelee kuwatumikia wananchi kwa weledi wa hali ya juu na kuhakikisha kero zote za awali zinatatuliwa, ikiwemo malalamiko ya wananchi kuhusu utolewaji wa Hati za kusafiria kiholela kwa misingi ya kisiasa na rushwa, na kuagiza uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu madai hayo na kuwasilisha Wizarani ripoti ya uchunguzi katika taarifa yake ya awali wiki hii.

0 comments:

Chapisha Maoni