Zoezi la kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo yasiyo ruhusiwa kisheria linatarajiwa kuhamia mkoani Arusha wakati wowote kuanzia sasa na wananchi wakiwemo waliojenga kwenye vyanzo vya maji wameshaanza kupewa taarifa.
Imeshuhudiwa kazi ya kuweka alama kwenye nyumba zilizojengwa kwenye vyanzo vya maji katika wilaya ya Arumeru zikiwekewa alama na wananchi wakitakiwa kuanza kuzibomoa wenyewe ili kunusuru mali zao.
Hata hivyo baadhi ya wananchi hao wameiomba serikali kutumia vyombo vyake kuwawajibisha watendaji wa serikali waliochangia na kuruhusu maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kujengwa na ikiwezekana walipe hasara inayojitokeza kwani wamefanya hivyo wakiwa wanajua wazi kuwa ni kosa.
Baadhi ya viongozi wa kata ikiwemo ya Kerai, Bw John Edward ambaye ni diwani pamoja na kukiri kuwepo kwa watendaji wanaoshiriki kuwasababishia wananchi hasara ameitaka serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi ambao walikuwepo kwenye maeneo hayo kabla ya sheria kupitishwa.
Arumeru ndio wilaya yenye vyanzo vya maji vinavyotegemewa na asilimia kubwa ya wananchi wa jiji la Arusha, na wilaya za jirani ikiwemo Monduli na Longido na ni miongoni mwa zinazokabiliwa na tatizo kubwa ya uharibifu wa mazingira.



0 comments:
Chapisha Maoni