Jumanne, Septemba 02, 2014

LEO KATIKA HISTORIA: JAPAN YASALIMU AMRI KATIKA VITA KUU YA PILI YA DUNIA

Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, yaani tarehe Pili Septemba mwaka 1945, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilifikia tamati baada ya Japan kusalimu amri bila ya masharti yoyote. Baada ya Japan kushindwa mfululizo na majeshi ya waitifaki, ililazimika kusalimu amri katika vita hivyo, hasa baada ya miji yake miwili mashuhuri ya Hiroshima na Nagasaki kushambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki. Baada ya tukio hilo lililotokea miezi minne tu baada ya kusalimu amri Ujerumani, nchi waitifaki ziliikalia kwa mabavu Japan kwa mujibu wa Mkataba wa Potsdam na Generali wa Kimarekani Douglas MacArthur akachaguliwa kuwa kamanda mkuu huko Japan. Mwaka 1951, nchi 49 duniani, zilitiliana saini mkataba wa amani na Japan, na mwaka mmoja baadaye nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikaanza kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe. 
NA....
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, nchi ya Vietnam ilipata uhuru. Vietnam ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa katikati mwa karne ya 19. Mwaka 1940 nchi hiyo ikadhibitiwa na Japan baada ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Vietnam iliendelea kuwa chini ya utawala na udhibiti wa Japan hadi pale Japan iliposalimu amri mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

0 comments:

Chapisha Maoni