Mwanamuziki maarufu ambaye pia ni mbunge nchini Somalia, Saado Ali
Warsame amepigwa risasi na kufa na wanamgambo. Aliuawa pamoja na mlinzi
wake, katika shambulio la kutumia gari mjini Mogadishu. Msemaji wa kundi
la al-Shabaab, Abdulaziz Abu Musab ameiambia BBC kuwa ameshambuliwa
kutokana na sababu za kisiasa na sio muziki wake. Mwandishi wa BBC mjini
Mogadishu Mohammed Moalimu amesema huyu ni mbunge wa nne kuuawa mwaka
huu. Bi Warsame alipata umaarufu enzi za
utawala wa rais wa zamani Siad Barre, aliyeondolewa madarakani mwaka
1991. Aliishi uhamishoni nchini Marekani kwa muda mrefu na alirejea
mwaka 2012 na kuwakilisha ukoo wake katika bunge jipya la Somalia.
Mwandishi wa BBC Idhaa ya Kisomali Abdullahi Abdi anasema Bi Warsame
atakumbukwa zaidi kwa muziki wake. Alikuwa mmoja wa wasomali wanawake
wachache aliyepanda jukwaani bila kujifunika kichwa na mara nyingine
kuvaa suruali, jambo ambalo sio la kawaida kwa wanawake wa Somalia,
amesema Abdi.
0 comments:
Chapisha Maoni