Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), limewataka
wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kurudi bungeni bila
masharti na kuendelea na mjadala wa Katiba kwa manufaa ya taifa.
Pia, Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of
God (TAG), Jimbo la Mashariki Kaskazini, Geoffrey Massawe amewaomba
wajumbe wa Bunge la Katiba kuungana na kuwa kitu kimoja katika mchakato
wa kujadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
Kauli hizo za maaskofu hao zimekuja siku moja
baada ya ile ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kusema kuwa hatima ya
uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu utategemea Ukawa, kurejea katika
Bunge Maalumu kuipitisha Katiba Mpya kwa wakati.
Askofu Massawe alitoa ombi hilo wakati wa ibada
maalumu ya sherehe ya maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa
kanisa hilo nchini iliyofanyika katika Kanisa la TAG Kinondoni, Dar es
Salaam.
Akitoa salamu za TEC wakati wa kuadhimisha miaka
25 ya uaskofu ya Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa kwenye Uwanja wa
Kichangani, Iringa, Makamu Rais wa TEC, Mhashamu Severine Niwemugizi
alisema ni vyema wajumbe hao wakarudi kwenye Bunge hilo linalotarajia
kuanza Agosti 5, mwaka huu.
0 comments:
Chapisha Maoni