WAKATI msafara wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars ukitarajiwa
kurejea nchini kesho ukitokea kambini nchini Botswana, kuna habari kuwa
Kocha Mart Nooij, amemtema mshambuliaji Mrisho Ngasa kwa utovu wa
nidhamu.
Hiyo ni baada ya nyota huyo kushindwa kusafiri na wenzake nchini
Botswana na kwenda nchini Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza
soka ya kulipwa na kufuzu, hivyo kusubiri baraka za klabu yake ya Yanga.
Chanzo cha uhakika kilichopo karibu na Nooij, kimedokeza kutoka
Botswana kwamba kocha huyo amemtema Ngasa kutokana na kukerwa na kitendo
chake cha kushindwa kutambua nafasi yake kwa Stars kuelekea mechi ya
Julai 20 dhidi ya Msumbiji.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa kitendo cha nyota huyo kushindwa
kuungana na wenzake, hivyo kukosa mazoezi muhimu kuelekea mechi hiyo
dhidi ya Msumbiji, kocha haoni sababu ya kuendelea kumng’ang’ania kwani
suala la timu ya taifa linahitaji utashi binafsi.
Stars itawakaribisha Msumbiji katika mechi ya kwanza kati ya mbili za
kuamua timu ya kuingia katika kundi F, kuungana na Zambia, Niger na
Cape Verde katika mbio za kuwania tiketi ya fainali za Mataifa Afrika
mwakani nchini Morocco.
Katika hatua nyingine, Stars inatarajia kurejea nchini saa 12:15
jioni na kuendelea kujifua kwa mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam.




0 comments:
Chapisha Maoni