Jumanne, Juni 24, 2014

UMEMALIZA MTAA MZIMA, NANI AKUOE???

Kweli tuna macho lakini  hatuoni, tuna masikio lakini hatusikii, tukiitwa masanamu tutakasirika? Nasema tena kwa mdomo mpana, baadhi yetu wanawake ni masanamu yenye damu. Hata ukinichukia ndiyo hivyohivyo kama wewe ni mmoja wao unatakiwa kubadilika.
Ujinga wetu wa kutotambua makusudi ya Mungu kukufanya mrembo, alikusudia kukurahisishia uonekane kwa urahisi na ili upate mume wa kukuoa.
Uzuri wako unautumia vibaya mwisho wa siku mnafanya  kila kona ya mji mabango ya waganga  wa kienyeji yaongezeke kukudanganyeni kuna  dawa za mapenzi pia kukufanya uolewe.
Nakuuliza unakwenda kwa mganga ili uolewe nani kakuroga? Usinitumbulie mimacho kama dume la panya lililonaswa na mtego, nakuuliza wewe acha kuangalia pembeni.
Ulipokuwa ukipendwa hukutaka kuolewa, wanaume wakija unaona wanataka kukufuja kwani ule ndiyo wakati wako wa kuvunja mifupa ili uzeeni uwasimulie wajukuu zako.
Dada weee, wanaume nao hawapigiwi, hawajapigiwa wanacheza ukiwapigia unafikiri nini kitakachofanyika, utagombaniwa kama mpira wa kona na kujiona upo juu kumbe popo ukijisaidia unajichafua mwenyewe. Mwanaume akiwa na shida na kitu yupo radhi hata kuuza nyumba ya urithi  ili tu akupate, si unalipa wakati huo. 
Lakini uzuri haukai milele na mwili wa kuchezewa sana unapoteza mvuto  na heshima mtaani, unajikuta ukiitwa majina ya kebehi Ooh, godoro la wanafunzi, mama huruma, jamvi la wageni au Call Box kila mwenye uwezo hujisevia.
Waswahili wanasema muda hausimami, kila uvutapo pumzi hesabu dakika inakwenda, umri unasogea uzuri nao unapotea. Pia haohao waswahili hawakukoma waliposema uanike wakati wa jua likiwa kali lakini ukicheza nalo utautwanga mbichi.
Walikuwa na maana nzito hasa kwetu wasichana kuutumia usichana wetu vizuri hasa pale tunapopata nafasi ya kutaka kuolewa kutokana na Mungu kutujalia sura na maumbile.
Kuna dada mmoja ambaye wakati sisi ndiyo tunapevuka alikuwa akitetemesha mtaa, kila mwanaume aliyemuona alitaka urafiki, wenye fedha walishindana kutangaza ndoa. Badala ya kuchagua mwanaume mmoja amuoe atulie, yeye aliona fahari kuwabadili kama nguo. Mwanaume gani hakuujua mwili wake.
Baada ya kuugawa hovyo mwili wake kila mtu alimdharau, hakuna aliyemfuata baada ya kujua ni maharage ya Mbeya. Matokeo yake akawa uwanja wa mazoezi kwa wapenda ngono, hakutofautiana na changudoa.
Baadaye aliposhtuka, alishachelewa, alitaka kuolewa  lakini sifa yake mbaya hakuna mwanaume aliyejitokeza. Baada ya kujiona amedoda akawa kila siku kwa waganga kutafuta dawa ya mvuto, kweli wanaume alipata lakini hakukuwa na muoaji.
Kila siku fedha yake iliishia kwa waganga lakini sifa yake ndiyo iliyomkosesha wanaume.Nani akuoe nawe kishata mtaa? Kwa tabia hizi tutazidi kujazana mabarazani kusubiri kuchukua waume wa wenzetu.

0 comments:

Chapisha Maoni