Wananchi wa kata ya Magara katika wilaya ya Babati mkoani Manyara,
wamelalamikia ukosefu wa daraja katika mto magara, licha ya ahadi za
mara kwa mara za kujenga daraja zilizotolewa na wagombea uraisi wa vyama
mbalimbali hali inayosababisha wanafunzi kusoma wakati wa kiangazi
pekee kutokana na wakati wa masika mto kujaa maji na wananchi na
wanafunzi kushindwa kuvuka upande wa pili kufuatia mto huo kujaa na
hivyo kutoruhusu magari na watu kuvuka.
Wananchi hao wamesema, ukosefu wa daraja katika eneo hilo,
unakwamisha kwa kiasi kikubwa shughuli za maendeleo na wakati mwingine
husababisha maafa na hasara kutokana na watu na magari kusombwa na maji
huku wanafunzi na wagonjwa wakishindwa kupata huduma kutokana na
kutokuwepo kwa uwezekano wa kuvuka upande wa pili ambapo wameiomba
serikali kujenga daraja katika mto huo ili kuharakisha maendeleo.
Kwa upande wake mkuu wa idara ya ujirani mwema katika hifadhi ya
taifa ya ziwa manyara Ibrahim Ninga amesema ukosefu wa daraja katika
mto huo unaopeleka maji yake katika ziwa manyara ni kikwazo kwa sekta ya
utalii kutokana na watalii kutoweza kuitumia barabara hiyo na kwamba
kutokana na tatizo hilo hifadhi ya ziwa manyara imejenga bweni la
wasichana katika shule ya sekondari magara ili kuhakikisha watoto wa
kike wanasoma muda wote.
0 comments:
Chapisha Maoni