Lugha ya kufundishia Sekondari ni Kiingereza. Wadau wengi wanasema hii
ni sababu moja ya vijana kutoelewa/kufeli. Tufundishe kwa Kiswahili?
Sote tunatambua kwamba Elimu ndio nguzo muhimu kwa maendeleo na katika
kurekebisha Elimu yetu suala la lugha ni muhimu. Tutafakari pia msingi
wa elimu ni nini hasa? Msingi wa elimu ni kupata maarifa na kuyatumia
kujiendeleza na kujenga jamii. Sababu ya elimu ni kupata maendeleo.
Elimu sio kwa ajili ya ajira tu. Shabaha ya elimu pia ni kujenga
udadisi na ubunifu katika kutafuta majawabu ya changamoto ndani ya
jamii. Je maarifa hayawezi kupenyezwa kwa Kiswahili? Tukisema Kiswahili
hakijitoshelezi maana yake tunakatia tamaa uwezekano wa kukipanua?
Katika nchi ndogo lakini zilizoendelea - Sweden, Norway, Denmark,
Finland - lugha zilizotumika kuvumbua mambo ni zao. Hii haiwezekani hapa
kwetu? Je ni kweli watu hufikiria kwa lugha yake ya asili?
Ukimlazimisha mtu afikirie, abaini na avumbue kwa lugha isiyo yake
ataweza au ataiga tu? Lugha sio kwa ajili ya mawasiliano tu na
walimwengu wengine. Lugha pia ni kwa ajili ya kujenga fikra na
kujitambua. Elimu haina majibu ya shida zote za jamii. Na elimu ya
kukaririsha majibu haifai. Elimu inapaswa kujenga uwezo na maarifa ya
kutafuta MAJAWABU.
0 comments:
Chapisha Maoni