Wingu jeusi limeanza kutanda kuhusu hatima ya mzozo wa Ziwa
Nyasa kutokana na msimamo wa hivi karibuni wa kiongozi wa Democratic
Progressive Party (DPP), Peter Mutharika ambaye sasa ni Rais mpya wa
Malawi.
Hiyo inatokana na msimamo wa Mutharika ambaye ni
Profesa wa Sheria wa kupinga kuendelea kujadiliana na Tanzania kuhusu
nani mwenye haki ya kumiliki ziwa hilo alioutoa wakati alipowatembelea
wananchi wa Chipoko, kando ya ziwa hilo miezi michache kabla ya uchaguzi
mkuu ambao ulimwigiza madarakani.
Pamoja na kwamba mazingira ya msimamo huo yanaweza
kutofautiana na hali halisi ya sasa, tofauti za kisiasa baina yake na
mtangulizi wake, Joyce Banda zinaweza kuongeza msukumo mpya wa kutaka
kutoendelea na mazungumzo ya mpaka wa ziwa hilo.
Akizungumza na wananchi hao, Profesa Mutharika
aliwatoa wasiwasi na kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa
maelezo kuwa ziwa hilo lipo kwenye himaya ya Malawi na kwamba kuendelea
kujadiliana na Tanzania ni kupoteza muda.
Hakuna haja ya kuendelea kujadiliana, Ziwa Malawi ni mali ya Malawi na litaendelea kuwa la Malawi daimaalisema Mutharika ambaye pia amewahi kufundisha sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alimshutumu Banda na kudai alikuwa dhaifu kiasi cha kutoa fursa kwa Tanzania kutumia udhaifu huo kutaka kupora ziwa hilo.
Ziwa hili letu ila Tanzania inatumia tu udhaifu wa Serikali iliyopo kwani wenyewe wanajua ndani ya mioyo yao kuwa hawana chochote katika ziwa hilo. Tutakaporejea serikalini mwakani haya mambo yote yasiyo na kichwa tutayamaliza. Nataka niwahakikishie kwamba tutapeleka meli zaidi kwenye ziwa hili ili kuinua shughuli zetu za kiuchumi na kutengeneza ajira kwa vijana wetu.
Hata hivyo, wiki iliyopita Serikali ya Tanzania
ilitoa msimamo wake kuhusu mzozo huo wa mpaka na kudaia kuwa itaendelea
kujadiliana na Malawi.
Akizungumza bungeni wakati akiwasilisha Bajeti ya
wizara yake, Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe alisema Tanzania ilikuwa ikifuatilia kwa karibu uchaguzi
wa Malawi na kwamba iko tayari kufanya kazi na serikali yoyote
itakayoingia madarakani.
0 comments:
Chapisha Maoni