Mashabiki wa soka wa Tanzania, jioni leo wameondoka uwanjani kifua
mbele baada ya kuishuhudia timu yao ya Taifa, Taifa Stars, ikiibuka na
ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zimbawe, mechi iliyopigwa katika Uwanja wa
Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mechi ya Stars na Zimbabwe ni ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la
Mataifa ya Afrika yatakayofanyika mwaka 2015, ambapo Stars imejiweka
katika nafasi nzuri kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa wiki mbili
zijazo nchini Zimbabwe.
Bao la Stars lilifungwa dakika ya 13 na John Bocco, huku akilifunga
kwa shuti kali nje ya 18, akitumia vyema pasi ya Thomas Ulimwengu.
Awali mpira ulianza kwa kasi, kila timu ikisaka bao la mapema katika
mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa kutoka kwa timu hizo.
Nyota wa Stars wakiongozwa na Mbwana Samatta, Ulimwengu, Bocco na
Mrisho Ngassa na wengine walifanya juhudi kuibuka na ushindi katika
mechi hiyo iliyokuwa na msisimko wa aina yake.
Dakika ya 13 Bocco anaipatia Stars bao la kwanza akipiga shuti kali nje ya 18, akitumia vyema krosi ndefu ya Ulimwengu.
Hata hivyo, mpira ulikuwa ukichezwa kwa rafu za kuvizia, huku mwamuzi
Joseph Odartel wa Ghana, kuwa mkali kwa wachezaji wote, akiwamo Milton
Mkude aliyeonyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Samatta.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Stars walitoka kifua mbele kwa kupata bao hilo moja lililofungwa na Bocco.
Dakika ya 46, Bocco alikosa bao la wazi kutokana na kufanya papara
wakati anauwahi mpira na kujikuta akianguka chini. Bocco alishindwa
kuitumia krosi ya Ulimwengu.
Wakati Stars wanaendelea kusaka bao jingine, walijikuta Ulimwengu
naye akionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi aliyeonyesha umakini na ukali
kwa wachezaji waliokuwa wakicheza rafu.
Kipindi cha pili Zimbabwe walirudi kwa kasi wakitaka kusawazisha,
lakini walishindwa kutokana na uimara wa wachezaji wa Taifa Stars.
Zimbabwe walifanya mabadiliko kwa kumtoa Peter Moyo na kuingia
Kudakwashe Musharu, lakini mabadiliko hayo hayajazaa matunda kwao, zaidi
ya kushuhudia mchezaji wao Stephen Alimenda akionyeshwa kadi ya njano
baada ya kumchezea madhambi Mwinyi Kazinmoto.
Kocha wa Stars, Mart Noij alimtoa Fank Domayo na kuingia Amri Kiemba,
wakati Mrisho Ngassa alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Haruna
Chanongo, huku Bocco akitoka na nafasi yake kuingia Khamis Mcha.
Hadi mwisho wa mchezo huo Stars walifanikiwa kutoka uwanjani kwa
ushindi wa bao 1-0, huku ushindi huo ukiiweka pazuri timu hiyo kwa mechi
ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo nchini Zimbabwe.
Stars: Deogratius Munish, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Nadir Haroub
Cannavaro, Kelvin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto,
Jonh Bocco, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Zimbabwe: George Chigova, Partson Jaure, Danny Phiri, Hardlife
Zvirekwi, Stephen Alimenda, Tendai Ndoro, Milton Mkude, Kudakwashe
Mahachi, Cuthbert Malajila, Peter Moyo na Eric Chipeta.
0 comments:
Chapisha Maoni