Jumatatu, Mei 26, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA...MEI 26

Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia wakati Waislamu walipokuwa chini ya mzingiro wa washirikina wa Makka. Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine huko katika Shiibi Abi Twalib. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu alipokuwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake Abdul Muttalib. Abu Twalib alisilimu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Mtukufu dhidi ya washirikina wa Kikureishi.

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, muafaka na tarehe 26 Mei mwaka 1981, kulitangazwa rasmi kuasisiwa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Baraza hilo linazijumuisha nchi 6 za kusini mwa Ghuba ya Uajemi ambazo ni Saudi Arabia, Kuwait, Baharain, Imarati, Qatar na Oman. Malengo ya baraza hilo yalitangazwa kuwa ni kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kusaidia kukabiliana na vitisho vya kigeni.

Na miaka 106 iliyopita kama leo sawa tarehe 5 Khordad mwaka 1287 Hijiria Shamsia, kisima cha kwanza cha mafuta cha Iran kilianza kutoa mafuta katika mji wa Msikiti wa Suleiman katika mkoa wa Khozestan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Kisima hicho kilichokuwa na urefu wa mita 600 kilianza kutoa mafuta ambayo yalijaa hadi mita 25 kutoka ardhini. Mji wa Masjid Suleiman una utajiri mkubwa wa madini na mafuta na hadi sasa zaidi ya visima vya mafuta 250 vimechimbwa katika mji huo. Si vibaya kukumbusha hapa kwamba, Iran ina utajiri mkubwa wa mafuta suala ambalo limeifanya ihesabiwe kuwa miongoni mwa nchi muhimu duniani. Pia baada ya Russia Iran ni nchi ya pili kuwa na utajiri mkubwa zaidi wa gesi duniani.

0 comments:

Chapisha Maoni